SHIRIKISHO la Vyama Vya Wafanyakazi Tanzania (TUCTA) limeainisha mambo matano yanayohitaji hatua za haraka kwa ajili ya kufanyiwa kazi kwa ustawi wa wafanyakazi nchini.
Masuala hayo yamewasilishwa mbele ya Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu,(Kazi, Vijana, Ajira Ajira na Wenye Ulemavu), Ridhiwan Kikwete na Katibu Mkuu wa TUCTA, Henry Mkunda katika mkutano mkuu wa nane wa Shirikisho uliofanyika jijini Dodoma.
Ameyataja masuala hayo kuwa ni mabadiliko ya Sheria za Kazi katika Utumishi wa Umma na athari zake kwa Wafanyakazi wa Sekta ya Umma.
Amesema mwaka 2018/19, Sheria ya Utumishi wa Umma (Sura 298) rejeo la 2019 ilifanyiwa marekebisho yanayomnyima mtumishi wa umma haki ya kutumia mfumo wa Tume ya Usuluhishi na Uamuzi (CMA) na Mahakama katika kutatua mgogoro wa kikazi.
“Mabadiliko hayo yameleta athari kubwa kwa watumishi wa umma. TUCTA tunapendekeza milango ya majadiliano ifunguliwe ili yafanyike marejeo ya Sheria hiyo lengo likiwa Mtumishi wa Umma kurejeshewa haki yake ya kuamua mfumo atakaoona unafaa kutatua mgogoro wake,” amesema.
Jambo lingine lililobainishwa ni Pamoja na uwiano wa malipo ya mkupuo kwa wastaafu yaani kikokotoo kwa Sekta ya umma na binafsi.
Ameipongeza Serikali kwa kusikiliza kilio cha wafanyakazi na kukubali kuboreshwa kwa kikokotoo cha malipo ya mkupuo kwa
Wastaafu na kwamba hoja yao ni kuwa maboresho yanaonesha
kunufaisha zaidi sekta ya umma ambayo kiwango chao cha malipo ya mkupuo kimepanda hadi asilimia 40 wakati kwa
sekta ya binafsi kimeishia asilimia 35.
Amesema tofauti iliyopo kwenye uwiano huo inaleta hisia za upendeleo na kwamba TUCTA inashauri milango ya mashauriano ifunguliwe ili jambo hilo lijadiliwe na muafaka upatikane.
Kuhusu ukosefu wa ajira nchini amesema kiwango cha ukosefu wa ajira kinaongezeka mwaka hadi mwaka. Ukosefu wa ajira ni mkubwa zaidi kwa vijana wenye umri kati ya miaka 21 hadi 45.
“TUCTA tunatambua kuwa, suala la ukosefu wa ajira sio kwa Tanzania peke yake bali la nchi nyingi Afrika na Duniani. Hoja ya TUCTA ni Serikali kuchukua hatua ya kupunguza tatizo la ukosefu wa ajira kwa Vijana.” amesema.
Amesema TUCTA inapendekeza kuanzishwa kwa miradi mingi
ya Serikali kadri iwezekanavyo ili iajiri sehemu kubwa ya Vijana
wanaozunguka kutafuta ajira kupitia miradi hiyo.
Kadhalika amesema TUCTA inapenda kuona mchakato wa ajira unakuwa wa wazi ili kuondoa hisia za upendeleo na ubaguzi
kwenye ajira.
Amesema pia wanashauri Serikali kuwa macho kwenye utekelezaji wa Sera ya Ajira ya Wageni kwani kuna dalili za wazi za ukiukwaji wa Sera hiyo.
Aidha, amesema ukosefu wa ajira unawaweka watanzania kwenye hatari ya kutumikishwa kwa ujira mdogo na kazi zisizo za staha.
Kuhusu ufanisi wa vyombo vya mashauriano amesema TUCTA inaamini ushirikishwaji na mashauriano ndio njia iliyo bora katika kupata majawabu ya changamoto mbalimbali zinazohusu wafanyakazi.
“Sheria zetu za kazi zimeweka bayana vyombo vya mashauriano na suala zima la ushirikishwaji wa wafanyakazi. Hoja yetu ni ufanisi wa vyombo hivyo kwa maana ya kuitishwa mara kwa mara kwa mujibu wa Sheria na utekelezaji wa kazi yale yanayokubalika kwenye vikao hivyo,” amesema.
Kuhusu usimamizi na udhibiti wa mifuko ya hifadhi ya jamii baada ya kuanzishwa kwa chombo cha kusimamia na kudhibiti mifuko hiyo mwaka 2008, TUCTA inaamini Chombo hicho kilifanya kazi nzuri kwa mujibu wa malengo ya kuundwa kwake.
Aidha amesema mwaka 2018, Chombo hicho kilifutwa kwa sababu ambazo hazikuwa bayana kwa wadau na kwamba hata baada ya mifuko kuunganishwa bado wanaamini chombo cha kusimamia na kudhibiti mifuko iliyopo kina umuhimu mkubwa wa kuendelea kuwepo.
Amesema wanaamini Serikali itaona umuhimu wa kurejesha chombo hicho.