Apongeza Kasi ya Uandikishaji Halmashauri Chalinze, Mkoa wa Pwani
Ashukuru Vituo Kuongezwa Kutatua Tatizo La Umbali
Na Mwandishi Wetu
PWANI: WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi,Ajira, Vijana na Wenye Ulemavu ambaye pia ni Mbunge wa Chalinze, Ridhiwani Kikwete amefika kijijini Msoga, Chalinze kujiandikisha ili aweze kupiga kura Uchaguzi wa Serikali za Mitaa na Vijiji.

Uchaguzi huo utafanyika Novemba 27, 2024. Ridhiwani amejiandikisha kutimiza takwa la katiba ili apate nafasi ya kupiga kura.
Akizungumza baada ya kujiandikisha, Ridhiwani ameishukuru serikali kwa kuongeza vituo vya kujiandikisha baada ya wananchi kulalamika kwa kutembea umbali mrefu kufuata kituo cha kujiandikisha.
“Naishukuru na kuipongeza Serikali kwa uamuzi wa kutuongezea kituo.

“Kuna watu wanatoka Chalinze Mzee, Chahua walilazimika kutembea umbali mrefu kufuata kituo cha kujiandikisha. Lakini kwa uamuzi huu tunatarajia namba itaongezeka.
“Na matarajio ya wananchi kupata haki yao ya kupiga kura yapatikana. Nakupongeza msimamizi kwa niaba ya tume na serikali ,” amesema.
Pia Ridhiwani amepongeza hali ya utulivu katika kipindi hiki cha uandikishaji, kwa kusema, “Amani ni tunu yetu, na muhimu kujitambulisha nayo kwa vitendo na Watanzania wanathibitisha hili kwa vitendo,”.

Amesema uandikishwaji huo ulizinduliwa Oktoba 11, 2024 na Rais Samia Suluhu Hassan, umekuwa na mafanikio makubwa ambapo hadi sasa halmashauri ya Chalinze imefikia zaidi ya asilimia 80 na inaendelea.
Pia Kimkoa, Wilaya ya Mkuranga ikiendelea kufanya vizuri katika uandikishaji.
Amesema wananchi wamesifu taratibu zilizoandaliwa, usimamizi na sasa wako tayari kwa hatua iliyo mbele ya kuwachagua viongozi wa serikali.