Na Lucy Lyatuu
WAFANYABIASHARA 45 wa Tanzania ndio waliotumia soko la eneo huru la Biashara la Afrika (AfCFTA) kuanzia mwaka jana 2023 hadi sasa.
Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Sekta Binafsi nchini (TPSF) Raphael Maganga amesema hayo Dar es Salaam katika warsha ya mafunzo kwa wadau kuhusu fursa zilizopo AfCFTA.Warsha hiyo imeandaliwa na Baraza la Biashara la Afrika Mashariki (EABC).

Akizungumza Maganga amesema Tanzania ilijiumga na soko hilo mwaka 2021 na Kwamba biashara zimeanza kufanyika 2023 ambapo wafanyabiashara wanapeleka vitu tofautitofauti.
Amezitaja baadhi ya bidhaa zinazokwenda katika soko hilo kuwa ni mbolea, nafaka, Kahawa, katani,viungo na hata bidhaa za kilimo na mchele.
Amesema mbali na Kampuni hizo lakini wanataka wasukume zaidi kampuni ambazo zina ongeza thamani kwenye bidhaa zao, nazo ziweze kushiriki kwa kuwa Tanzania haitaki kuendelea kukuza malighafi Bali kukuza bidhaa ambazo zitaongeza ushindani.
“Lazima na sisi tuchangamkie, muda umefika biashara za Tanzania zitoke,tusiwaogope wenzetu tayari serikali imesaini mikataba mbalimbali hivyo muhimu kuzifikia fursa hizo,” amesema Maganga.
Aidha amewahamasisha Watanzania kutumia muda huo ambao wamepewa wa kipekee (GTI) wa nchi nane kuanza kupeleka bidhaa zao katika soko hilo badala ya kusubiria nchi zote 55 za Afrika kuanza.
‘Tanzania ni miongoni mwa nchi nane kati ya hamsini na tano za Afrika zilizochaguliwa kuanza kulitumia soko hilo,ambapo ni fursa muhimu ili kampuni nyingi zijitokeze Kwa wingi,” amesema.
Kwa upande mwingine amezitaka kampuni za kitanzania kuchangamkia mtaji wa Dola bilioni moja uliotolewa na benkibya AfriExim Kwa ajili ya kuhakikisha zinafanya biashara katika soko hilo.
Kwa upande wake, Meneja wa Wanachama na Maendeleo ya Biashara kutoka EABC,Zefania Shaidi amesema lengo la warsha hiyo kujadili kuhusu mfumo mzima wa biashara katika soko hilo Kwa kuwa tayari wapo wafanyabiashara wanapeleka bidhaa nchi za Moroco,Aljeria na hata Nigeria.
Amesema wamewakutanisha wafanyabiashara ambao tayari wameanza kutumia soko hilo Ili watoe uzoefu wao pamoja na changamoto wanazokutana nazo Ili kutafuta ufumbuzi pia.