Na Lucy Ngowi
DAR ES SALAAM: KATIBU Mkuu wa Wizara ya Sayansi na Teknolojia, Profesa Carolyne Nombo amezindua Miongozo ya Kitaifa ya Usimamizi wa Utafiti na Ubunifu ya Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH).
Profesa Nombo amefanya uzinduzi huo Mkoani Dar es Salaam, katika hafla iliyoandaliwa na COSTECH.
Nombo ametaja mwongozo wa kwanza ni wa Kitaifa wa Ushirikiano kati ya Taasisi za Elimu ya Juu, Taasisi za Utafiti na Viwanda.
“Kwa muda mrefu kumekuwa na changamoto ya ushirikiano duni kati ya vyuo vikuu, taasisi za utafiti na sekta ya viwanda.
” Hali hii imesababisha tafiti nyingi ambazo zinaendelea katika taasisi zetu za elimu ya juu kutoendana na mahitaji ya viwanda au jamii yetu.
“Mwongozo huu unakusudia kutatua changamoto hiyo kwa kuweka kanuni, taratibu na miongozo itakayorahisisha ushirikiano wa karibu kati ya taasisi hizi,” amesema.
Mwingine ni Mwongozo wa Kitaifa wa upatikanaji, uhifadhi na usambazaji wa takwimu za sayansi, teknolojia na ubunifu.

Amesema mwongozo huo unalenga kuimarisha upatikanaji, uchakataji, uhifadhi na usambazaji wa takwimu za sayansi na teknolojia kwa ufanisi zaidi.
Vile vile mwongozo wa Taifa wa uwezo wa utafiti wa kisayansi na nne ni Mwongozo wa Kitaifa wa ubunifu.
Amesema utafiti na ubunifu ni nyenzo muhimu katika kuchagiza maendeleo ya kiuchumi na kijamii, kwani nchi zote zilizoendelea duniani zimefanikiwa kutokana na uratibu na uwekezaji madhubuti katika masuala hayo.
Profesa Nombo amesema kupitia Mradi wa Mageuzi yaKiuchumi kupitia Elimu ya Juu (HEET), serikali imewekeza dola za kimarekani milioni 425 sawa na Sh. Trilioni 1.1 katika miundombinu ya elimu, vifaa vya kisasa vya kufundishia, kuimarisha ushirikiano baina ya vyuo vikuu na sekta ya viwanda.
Naye Mkurugenzi Mkuu wa COSTECH Dkt. Amos Nungu amesema tume hiyo ni miongoni mwa wanufaika 23 wa mradi wa HEET, ambao katika tume hiyo umelenga kuimarisha ujenzi na ukarabati wa miundombinu ya sayansi, teknolojia na ubunifu.
Pia amesema mradi huo umelenga kukuza na kuendeleza uwezo wa utafiti na ubunifu katika taasisi za utafiti na maendeleo ya elimu ya juu.

Vile vile kujenga uhusiano wa kiutendaji kati ya sekta binafsi na taasisi za utafiti na maendeleo na elimu ya juu.
Ametaja eneo lingine ni kuboresha miundombinu ya kisasa ya tehama, vifaa vya huduma kwa ajili ya usimamizi wa utafiti na ubunifu.
Eneo lingine ni kukuza uwezo endelevu wa kugharamia utafiti na ubunifu, pamoja na kuimarisha uwezo wa tume katika kuratibu utafiti na ubunifu.