Na Mwandishi Wetu
TAASISI ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI), kupitia vituo vyake vitatu kwa Kushirikiana na watafiti kutoka Kituo cha Kimataifa cha Utafiti wa Fiziolojia na Ikolojia ya wadudu (ICIPE) kilichopo Kenya, imetoa mafunzo kwa wadau juu ya kudhibiti wadudu waharibifu wa matunda.
Vituo hivyo vya TARI ni Ukiriguru (Mwanza), Tengeru (Arusha) na Mlingano (Tanga) ambavyo vimetoa mafunzo hayo kudhibiti wadudu waharibifu kwenye matunda aina ya parachichi, machungwa na embe.

Mafunzo hayo yamefanyika Septemba tisa hadi 13, mwaka huu katika Wilaya za Hai, Siha Mkoani Kilimanjaro pamoja Muheza, Mkoa wa Tanga ikiwa ni utekelezaji wa mradi wa njia husishi za kudhibiti wadudu wa miti ya matunda kwenye ikolojia mbalimbali.
Mtafiti Kiongozi wa Mradi huo kutoka TARI Ukiliguru, Dkt. Abdulla Mkiga amesema katika wilaya za Hai na Siha walijikita katika matunda ya parachichi, huku kwa Wilaya ya Muheza mafunzo yalijikita kwenye matunda ya machungwa na embe.
Amesema lengo la mafunzo ni kuhakikisha wakulima wanapata elimu bora ya kudhibiti wadudu waharibifu wa matunda kama nzi na nondo wanaoshambulia matunda ambao husababisha matunda kuoza na kushusha kiwango cha mavuno na ubora.
Kwa upande wake mtafiti kutoka ICIPE Dkt. Shepard Ndlela amesema kupitia njia husishi za kudhibiti visumbufu mkulima ataweza kupunguza gharama na matumizi ya viuadudu vya kemikali na kuongeza mavuno na ubora kwa soko ndani na kimataifa.

Charles Semagongo mkulima wa machungwa Kijiji cha Mkinga, Wilaya ya Muheza amesema kupitia mafunzo hayo ameweza kuwatambua wadudu ambao awali alikuwa hafahamu kama ni hatarishi kwenye matunda.
Naye Fatuma Muhammed-Mkulima wa machungwa Kijiji cha Mkinga Wilaya ya Muheza, amesema mafunzo hayo yamewasaidia sio tu kutambua wadudu waharibifu bali pia kutambua wadudu rafiki kwenye uzalishaji wa matunda ambao awali walidhani ni hatarishi lakini Wataalamu wamewaeleza ni wadudu rafiki wanaozuia wadudu waharibifu kushambulia matunda na wanachangia kuongeza tija.
“Sisi tulijua hawa wadudu (jamii ya siafu) tunawaita huku kwetu “madadada” kuwa ni waharibifu wa machungwa lakini wataalamu wametueleza ni wadudu rafiki wanaozuia wadudu wengine kushambulia machungwa” amesema.
Awali wakati wa ufunguzi wa mafunzo hayo Wilayani Hai, Mkuu wa Wilaya hiyo Lazaro Twange aliipongeza TARI kwa kuweka nguvu katika kuwajengea uwezo wataalam wa kilimo na wakulima viongozi katika maeneo mbalimbali ikiwa ni sehemu ya juhudi za serikali kuinua sekta hiyo muhimu.
Kwa upande mwingine Mkurugenzi mtendaji wa Wilaya ya Muheza Dkt Juma Mhina amesema mradi huo umekuja wakati sahihi na kwa watu sahihi akitolea mfano wa Muheza kuwa Uchumi wa wananchi wa Wilaya hiyo hutegemea machungwa na wamekuwa na kilio cha wadudu waharibifu wa matunda hayo.

Dkt. Mhina amesema mradi huo utakuwa ni suluhisho la changamoto ya wadudu waharibifu huku ikichangia kipato cha wakazi wa Muheza, kuongezeka mapato ya Halmashauri na hatimaye taifa kwa ujumla kupitia Kilimo cha matunda yanayouzwa ndani na nje ya nchi.
Mradi huo unatekelezwa kwa miaka mitatu (2023-2026) kupitia kituo cha TARI Ukiriguru kwa kushirikiana na taasisi ya ICIPE chini ya ufadhili wa Shirika la Maendeleo la Ujerumani (GIZ).