Na Mwandishi wetu
MOROGORO: MENEJIMENTI ya Tume ya Utumishi wa Walimu (TSC) imeagizwa kufanya utafiti kubaini chanzo cha makosa ambayo yanawakumba walimu na kuwasababishia kuadhibiwa.
Kamishna wa tume hiyo, Mariam Mwanilwa amesema hayo alipokuwa akitoa maoni yake kabla ya kufungwa kwa mkutano wa siku tatu wa Tume hiyo uliolenga kuamua masuala mbalimbali ikiwemo rufaa za walimu.
Mwanilwa amesema katika kipindi cha siku tatu wamesikiliza na kutoa uamuzi wa jumla ya rufaa 16, kati ya hizo sita waliombwa kufika mbele ya tume kwa ajili ya kuongeza maelezo katika utetezi wao wa maandishi, rufaa hizo ziliwasilishwa kwa njia ya maandishi.

Amesema kuwa katika idadi hiyo walimu waliozaliwa kati ya mwaka 1980 hadi 1988 waliongoza kwa kutuhumiwa idadi yao ikiwa 11, waliozaliwa kati ya 1971 hadi 1979 walikuwa wawil, na mwaka 1990 hadi 1992 walikuwa wawili.
Amesema kwa kuangalia takwimu hizo ufanyike utafiti kuangalia aina ya makosa, umri na jinsi ambayo walimu wamekuwa wakituhumiwa kuyafanya zaidi.
Aidha, Kamishna huyo ameshauri kuongeza nguvu zaidi katika kutoa elimu kwa walimu kuhusu masuala mbalimbali yakiwemo ya nidhamu ili kuwaepusha kufanya makosa ambayo yanasababisha baadhi yao kufukuzwa kazi.
Naye Kamishna Jane Mtindya amesema hatua hiyo ya kufanya utafiti ni ya msingi kwani hata miaka ya nyuma walishaagiza kufanyika ambapo ilibainika kuwa vijana wengi waliozaliwa miaka ya 1990 waliamua kusomea Kada ya Ualimu kwa lengo la kupata mikopo ya elimu ya juu iliyokuwa ikitolewa na Serikali.