Na Lucy Lyatuu
CHAMA Cha Wanasheria Tanzania (TLS) kimesema mfumo wa uendeshaji na usimamizi wa mashauri kwa njia ya mtandao (OCMS) ni wa muhimu na wenye kuleta usawa na haki kwa wafanyakazi.
Ni mfumo utakaowaondoa watoa maamuzi ya kazi kwenye kutumia njia ya makaratasi katika kufungua mashauri mbalimbali na kwenda kwenye Dunia ya kidigitali zaidi.
Mjumbe wa Baraza la Uongozi Kanda ya Mzizima, Pilinga Panya amesema hayo Dar es Salaam katika mafunzo kwa wadau kuhusu mfumo huo ulioandaliwa na Tume ya Usuluhishi na Uamuzi (CMA)
Akizungumza amesema mafunzo kuhusu mfumo huo, ni ya muhimu Kwa wadau wa kazi na sheria nchini Kwa ujumla ambayo yatao esha Wanasheria na Wafanyakazi Tanzania namna ambayo CMA imejipambanua kwenda na kasi ya kidigitali.
Amesema kasi hiyo ni ya maendeleo na teknolojia Kwa kuwa mfumo huo ni wa kusimamia na kuendesha kesi Kwa njia ya kidigitali.
” Mfumo ambao mhimili waa Mahakama umeshaanza kuufanyia kazi na Wanasheria wengi wanafungua kesi Kwa mfumo wa kidigitali Mahakamani,’ amesema.
Amesema licha ya Mahakama kutumia mfumo kama huo lakini Kwa watoa usuluhishi na maamuzi walikuwa wanatumia njia ya zamani ya makaratasi na kuzunguka na mafaili Ila Kwa Sasa wamejipambanua kwenda na kasibya dunia.
Amesema mfumo utaleta tija,kupunguza gharama za watu wengi,utaokoa muda na hata kuweka kumbukumbu nzuri za kudumu zinazoweza kupatikana pindi zikihitajika kufanyika marejeleo.
Kwa upande wake Mwanasheria kutoka Taasisi ya Kuzuia Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Belinda Kiswaga amesema ni mfumo Shirikisho wenye kusukuma mashauri ya wafanyakazi na utakuwa wa Wazi kwa wadau wote na haki kupatikana kirahisi.