Na Lucy Ngowi
MVUA za vuli 2024 zinatarajiwa kuanza wiki ya nne ya Septemba katika ukanda wa Ziwa Victoria na kusambaa katika maeneo mengine katika wiki ya kwanza na ya pili ya Oktoba.
Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), Dkt. Ladislaus Chang’a amesema hayo Mkoani Dar es Salaam, alipokuwa akitoa mwelekeo wa Mvua za Vuli Oktoba hadi Disemba, 2024.
Dkt. Chang’a amesema mvua hizo zinatarajiwa kuongezeka kidogo kidogo Disemba mwaka huu.
Ameelezea athari zinazotarajiwa kutokea, ni pamoja na upungufu wa unyevunyevu katika udongo unatarajiwa kujitokeza katika maeneo mengi, hivyo kuathiri shughuli za kilimo.
“Kina cha maji katika mito na mabwawa vinatarajiwa kupungua. Kujitokeza kwa magonjwa ya mlipuko, kutokana na upungufu wa maji safi na salama.
“Vipindi vya joto kali kuliko kawaida vinatarajiwa katika msimu wa vuli. Uwepo wa La-Nina hafifu unatarajiwa kuwa na mchango mkubwa katika mvua za msimu wa vuli mwaka huu,” amesema.
Awali amesema mvua hizo zinatarajiwa kuwa za chini ya wastani hadi wastani katika maeneo mengi na zinatarajiwa kuanza kwa kusuasasua na kutawaliwa na vipindi virefu vya ukavu na mtawanyiko wa mvua usioridhisha.
Mvua hizo ni mahususi kwa maeneo ya Nyanda za Juu Kaskazini Mashariki ambako ni mikoa ya Arusha, Manyara na Kilimanjaro.
Pia Pwani ya Kaskazini, Kaskazini mwa mkoa wa Morogoro, Mikoa ya Pwani ikijumuisha Visiwa vya Mafia, Dar es Salaam, Tanga na Visiwa vya Unguja na
Pemba.
Ukanda wa Ziwa Victoria ambako ni mikoa yaKagera, Geita, Mwanza, Shinyanga, Siiyu na Mara, pamoja na Kaskazini mwa Mkoa wa Kigoma.