Na Lucy Lyatuu
WAZIRI wa Viwanda na Biashara, Dk Selemani Jafo, amesema bado ipo kazi kubwa ya kufanya Ili Kutumia kikamilifu fursa ya Mpango wa Ukuzaji wa Biashara Afrika na Marekani (AGOA).
Amesema kuna haja ya kuendelea kukuza na kuimarisha uwezo wa uzalishaji na ugavi ili kukidhi mahitaji ya soko, kubadilisha kiwango Cha mauzo ya nje kwa kupanua zaidi ya sekta na kujumuisha bidhaa zilizoongezwa thamani na viwango vya juu, na kuimarisha ustahimilivu wa ugavi kwa kujenga nguvu na ufanisi.
Hata hivyo serikali ya Marekani kupitia Shirika lake la Maendeleo (USAID), limesema litatoa uwekezaji wa dola milioni 8.3 kwa makampuni kadhaa ya Tanzania ili kukuza biashara, kuboresha usalama wa chakula.
Dk Jafo amesema hayo leo Dar es Salaam katika maonesho ya mradi wa biashara na Uwekezaji (ATI) kati ya Serikali ya Marekani kupitia USAID.
Amesema yapo mafanikio kupitia Mradi wa Biashara na Uwekezaji (ATI), ambao unathaminiwa sana, lakini bado kuna kazi kubwa ya kufanywa ili kutumia kikamilifu uwezekano wa biashara na uwekezaji nchini.
Amesema pia kuna haja ya kuimarisha miundombinu kwa kuwekeza katika usafirishaji, vifaa, na uunganishaji wa kidijitali ili kurahisisha biashara na kupunguza gharama, na kukuza uvumbuzi na ujasiriamali kwa kuhimiza maendeleo ya bidhaa na huduma mpya ili kukidhi mahitaji yanayoendelea katika soko la Marekani na kwingineko.
“Tunapoangalia siku za usoni, Serikali imejipanga kuendeleza kasi hii iliyofikiwa kupitia Mradi wa ATI, kuongeza juhudi zetu, na kuhakikisha kuwa manufaa ya mradi huu yanawafikia wananchi wengi zaidi kote nchini,” amesema.
Mkurugenzi wa Misheni ya USAID Tanzania Craig Hart amesema
Kupitia mradi huo utaimarisha ushindani wa Tanzania katika nyanja ya mauzo ya nje kupitia fursa ya soko la Marekani .
Amesema kampuni tisa za ndani zitapata ruzuku chini ya Mradi wa Biashara na Uwekezaji wa USAID Afrika.
Alizitaja baadhi ya kampuni hizo kuwa ni BioBuu, Biotan Limited, Central Park Beew, Minjingu Mines na Fertilizer Limited, Mount Meru Millers, na Red Earth Limited.
“Tunasherehekea ushirikiano wa USAID na makampuni tisa katika sekta muhimu, ikiwa ni pamoja na asali, korosho na nguo, ambayo yanatarajiwa kuzalisha ajira 2000, na kukuza hadhi ya Tanzania kama kitovu cha uchumi wa kanda,” amesema.
Amesema kupitia fursa ya Soko la Agoa, wanasaidia kampuni ya Kitanzania kutafuta masoko Amerika.
“Agoa ni sehemu muhimu ya sera ya kiuchumi ya Marekani na Afrika, inayozipa nchi zinazostahiki zilizo Kusini mwa Jangwa la Sahara upatikanaji bila ushuru katika soko la Marekani kwa bidhaa zaidi ya 1800,” amesema.