Mwandishi wetu. Senegal
UMOJA wa Afrika (AU), umeviomba vyombo vya habari Barani Afrika kuandika vizuri habari za Afrika ikiwepo masuala ya uhamaji wafanyakazi ndani ya Afrika na nje ya Afrika.
Kumekuwepo na ongezeko la uhamaji wa wafanyakazi kutoka watu 17.2 millioni mwaka 2010 hadi kufikia watu 26.3 millioni mwaka 2019.
Uhamaji huo wa wafanyakazi umeingiza mapato ya fedha za kigeni katika nchi za Afrika kutoka dola billion 55 mwaka 2010 hadi kufikia dola billion 86.4 mwaka 2019 hata hivyo kumekuwepo na upotoshwaji wa jambo hili hasa na vyombo vya habari vya nje.
Akizungumza katika warsha ya siku tatu ya kuwajengea uwezo viongozi wa wafanyakazi katika vyama vya waandishi wa habari Afrika, Wahariri na Waandishi waandamizi inayoendelea Dakar nchini Senegal,
Mkuu wa Kitengo cha Kazi, Ajira na Uhamaji katika Kamisheni ya Umoja wa Afrika, Dk Sabelo Mbokazi amesema vyombo vya habari vya Afrika vina wajibu kueneza ujumbe halisi kuhusu umuhimu wa uhamaji katika maendeleo ya nchi za Afrika.
Amesema kwa sasa kutokana na ukuaji wa teknolojia Duniani kumekuwepo na ongezeko la habari za uongo na upotoshwaji kuhusu bara la Afrika.
“Nyie kama viongozi wa wanahabari Afrika mnawajibu kusaidia kuandika mambo yenye manufaa kwa Afrika,” amesema.
Dk Mbokazi, pia alitoa wito kwa Waandishi wa Habari kuchukua jukumu kubwa katika kuhakikisha Kunakuwepo na mazingira bora ya Uhamiaji wa kazi barani Afrika.
Rais wa Shirikisho la Waandishi wa Habari Afrika (FAJ) Omar Faruk Osman amesema watendaji wa vyombo vya habari wanapaswa kutumia wingi wa vyanzo vyao ili kufichua ukiukaji wa kazi na kuboresha utawala wa Uhamaji wa Wafanyakazi barani Afrika.
Osman amesema, viongozi wa vyama vya wafanyakazi na wanahabari wanapaswa pia kuhamasisha waafrika kufanya kazi zenye staha nje ya nchi zao,kulipwa vizuri lakini kulindwa kwa haki zao.
Akitoa Takwimu juu ya uhamiaji wafanyakazi ndani ya Afrika na nje ya Afrika, Ofisa wa takwimu, katika kitengo Cha uhamaji wafanyakazi wa Umoja wa Afrika, Brian Okengo amesema kumekuwepo na ongezeko la uhamiaji wafanyakazi katika utafiti ambao umefanywa kuanzia mwaka 2010 hadi 2019.
Awali akifungua warsha hiyo, Mkurugenzi wa Mawasiliano wa Serikali ya Senegal, Ousseynou Dieng kwa niaba ya Waziri wa wa Mawasiliano, alitaka waandishi barani Afrika kuungana kuandika vizuri bara la Afrika.