Na Lucy Ngowi
DODOMA; WAKALA ya Barabara ya Vijijini na Mijini (TARURA), imewekeza maabara 10 katika mikoa mbalimbali nchini ili kusimamia utengenezaji bora wa barabara.
Fundi Sanifu Mkuu Maabara ya TARURA, Jacob Manguye amesema hayo katika maonesho ya Wakulima, Wafugaji na Wavuvi yanayoendelea viwanja vya Nzuguni Dodoma.
Amesema mbali na maabara iliyoko Dodoma, nyingine ziko mikoa ya Mbeya, Geita, Kigoma, Simiyu, Tanga, Mtwara na Mwanza.
Mikoa mingine ni Ruvuma, Morogoro, Arusha na Ilala Dar es Salaam.
Amesema ili barabara nzuri itengenezwe lazima ianzie maabara kwa kupima sampo za udongo, kokoto, lami ama bidhaa za ujenzi wa barabara.
“Barabara nyingi zinaharibika kwa sababu aidha watu hawapimi ili waweze kuoata uhakika kuwa udongo ule wanaotaka kujenga kwenye barabara unahimili.
“Maana yake ni kwamba magari yanapopita na uzito wake , barabara iweze kuhimili bila kubonyea au bila kusambaratika baada ya kutengenezwa,” amesema.
Amesema uwepo wa maabara hizo kwenye mikoa unarahisisha usimamizi ili kazi za tarura ziwe imara.