Na Mwandishi Wetu
Bodi ya Mkonge Tanzania (TSB), itazindua mradi mpya ujulikanao kama ‘Jenga Kesho Iliyo Bora kupitia Zao la Mkonge’ katika eneo la Koba Jimbo la Makunduchi, Zanzibar Julai 27, mwaka huu.
Mradi huo unalenga katika kuwajengea uwezo au kuwawezesha vikundi vya kinamama, vijana na watu wenye ulemavu kupata utaalamu wa kuzalisha bidhaa za Mkonge kwa kutumia mikono.
Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Mkonge, Saddy Kambona amesema hafla ya uzinduzi huo, itahusisha tukio la ugawaji wa Singa za Mkonge zipatazo tani 9.6.
Amesema mradi huu ni endelevu ambapo unategemewa ndani ya miaka mitano hadi kufikia mwaka 2030 uwe umeondoa tatizo la ukosefu wa ajira kwa takribani watu wasiopungua 10,000.
“Mradi huu unalenga kuongeza matumizi ya zao la Mkonge ndani ya nchi, kupanua wigo wa matumizi ya Mkonge, kupunguza Mkonge unaosafirishwa nje bila kuuongezea thamani ambapo hadi sasa asilimia 70 ya Mkonge wote unaozalishwa hapa nchini unasafirishwa nje bila kuongezewa thamani na hivyo kusababisha nchi kukosa mapato stahiki.
“Kwa hiyo tunafanya hivyo kuisaidia serikali kutatua changamoto ya ajira nchini na kubadilisha hali za watu wetu kwa sababu kupitia uzalishaji wa bidhaa za Mkonge wataweza kutumia vizuri Soko la Utalii Zanzibar na kujipatia kipato kwa kuuza bidhaa za nyuzi asilia,” amesema.
Katika mradi huo Zanzibar, TSB inashirikiana na Ofisi ya Kamishna wa Chuo cha Mafunzo, Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Unguja Kusini, Katibu Mkuu wizara ya Utalii na Mambo ya Kale, Katibu Mkuu wa Viwanda na Uchumi wa Buluu, Katibu Mkuu Maendeleo ya Jamii na wadau wengine katika kuhakikisha kwamba mradi huu unafanikiwa.0