Na Lucy Ngowi
WIKI ya kudhibiti bidhaa bandia duniani hapa nchini yanaadhimishwa kesho mkoani Dar es Salaam.
Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Ushindani (FCC), William Erio amesema hayo alipozungumza na waandishi wa habari leo.
Amesema maadhimisho hayo yenye kauli mbiu, ‘Kulinda bidhaa bandia kwa nia ya kulinda ubunifu na kukuza uchumi yalianza Julai 15, mwaka huu.
Amesema kukosekana kwa ushirikiano kutoka kwa wadau, wafanyabiashara pamoja na wananchi ndicho chanzo cha bidhaa hizo kuendelea kuwepo nchini.
“Tume ya ushindani inaendelea kutoa elimu juu ya madhara ya bidhaa bandia kwa kuandaa semina na midahalo mbalimbali lakini changamoto kubwa ni kukosa ushirikiano,
“Wafanyabiashara wanajua fika kwamba hizo bidhaa zinauzwa duka fulani lakini hawatoi taarifa zaidi wanafurahia kununua bidhaa kwa bei ya chini ili hali madhara yake ni makubwa,ni wakati wa ninyi wadau kutoa elimu ilituweze kudhibiti bidhaa hizi,” amesema.
Amesema bidhaa bandia zinasababisha kuzorota kwa biashara kwa kuwa bidhaa hizo hazifuati mifumo rasmi ya serikali hivyo kusababisha ukwepaji wa kodi na kuipa hasara serikali.
Maana yake ni kwamba mtu anayefanya biashara halali hawezi kushindana na mtu anayefanya biashara bandia sababu bidhaa zake ni za bei ya chini kuliko kawaida.
Pia amesema biashara bandia ina athiri uwekezaji kwa kuwa wawekezaji wanapotaka kuwekeza nchini ni lazima wafanye uchunguzi wakibaini kuna uingizwaji wa bidhaa bandia hawawekezi tena.