Dodoma Sekondari yapatiwa Sh milioni 198
Na Mwandishi Wetu, Dodoma
SHULE 167 za sekondari nchini zinatekeleza mtaala wa Elimu ya Amali unaolenga kuwajengea wanafunzi ujuzi wa vitendo utakaowawezesha kujiajiri, kujitegemea na kukidhi mahitaji ya soko la ajira.
Mkurugenzi wa Elimu ya Msingi wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Abdul Maulid, ameeleza hayo alipotembelea Shule ya Sekondari Dodoma kukagua ujenzi wa karakana na upatikanaji wa vifaa vya kujifunzia na kufundishia katika fani ya upishi na uandaaji wa chakula.

Shule hiyo imepatiwa ruzuku ya zaidi ya Sh. Milioni 198 kutoka Mfuko wa Elimu wa Taifa, unaosimamiwa na Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA), kwa ajili ya ujenzi wa karakana na ununuzi wa vifaa vya mafunzo hayo.
Maulid amesema Serikali kupitia TEA imetenga takribani Sh. Bilioni 3.8 katika mwaka wa fedha 2025/2026 kwa ajili ya ujenzi wa karakana na ununuzi wa vifaa vya kujifunzia na kufundishia katika shule 16 zinazotekeleza mtaala huo.
“Tunashukuru Serikali kupitia TEA kwa kutoa takribani Sh. Bilioni 3.8 katika mwaka wa fedha 2025/2026 kwa shule 16 kwa ajili ya ujenzi wa karakana na ununuzi wa vifaa vya kujifunzia na kufundishia katika shule zinazotekeleza mtaala huu,” amesema.
Kwa upande wake, Mkuu wa Shule ya Sekondari Dodoma, Francis Tumaini, amesema upatikanaji wa vifaa hivyo utaimarisha mafunzo ya vitendo na kuwapa wanafunzi ujuzi utakaowawezesha kujiajiri baada ya kuhitimu.

Amesema mafunzo hayo ni muhimu katika kuwaandaa wanafunzi kutumia ujuzi wanaoupata kuanzisha shughuli za kiuchumi na kujitegemea.
Maoni 0
Hakuna maoni bado. Kuwa wa kwanza kutoa maoni!