Nenda moja kwa moja kwenye maudhui
November 6, 2026
Habari Lucy Ngowi 8

WyEST Na TEA Wakagua Miradi Ya Elimu Ya Amali Ya Sh. Milioni 347.5 Morogoro

Na Mwandishi Wetu

WIZARA ya Elimu, Sayansi na Teknolojia (WyEST), kwa kushirikiana na Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA), imekagua miradi miwili ya elimu ya amali katika Shule za Sekondari Mafiga na Morogoro, yenye thamani ya Sh. Milioni 347.5.

Miradi hiyo inayofadhiliwa na Mfuko wa Elimu unaosimamiwa na TEA inalenga kuboresha mazingira ya ufundishaji na ujifunzaji kwa kuimarisha vifaa na miundombinu ya mafunzo ya vitendo.

Habari Picha 14196

Shule ya Sekondari Mafiga, inayofundisha amali ya kilimo, imepatiwa Sh. Milioni 280.8 kwa ajili ya ununuzi wa vifaa na mitambo ya kufundishia, ikiwemo trekta.

Nayo Shule ya Sekondari Morogoro imepatiwa Sh. Milioni 66.65 kwa ajili ya ujenzi wa uwanja na jukwaa la mpira wa pete.

Habari Picha 14197

Akizungumza baada ya ukaguzi huo, Msaidizi wa Kamishna wa Elimu kutoka WyEST, Suzana Raphael, ameipongeza TEA kwa kuwezesha upatikanaji wa vifaa na miundombinu inayosaidia utekelezaji wa mtaala wa elimu ya amali.

Amesema wizara itafanyia kazi changamoto zilizobainika ili kuboresha mazingira ya ufundishaji na ujifunzaji.

Habari Picha 14199

Mkurugenzi wa Utafutaji Rasilimali na Usimamizi wa Miradi ya Elimu wa TEA, Masozi Nyirenda, amesema mamlaka hiyo itaendelea kuunga mkono miradi ya elimu ya amali ili kuwawezesha wanafunzi kupata ujuzi unaokidhi mahitaji ya soko la ajira na kuongeza fursa za kujiajiri na kuajiriwa.

Mkuu wa Shule ya Sekondari Mafiga, Robert Marwa, ameishukuru Serikali kupitia WyEST na TEA kwa vifaa vya kilimo vitakavyoboresha mafunzo ya vitendo.

Naye Hussein Hussein amesema elimu ya amali imeongeza mwamko kwa wanafunzi na wazazi, huku vifaa hivyo vikitarajiwa kusaidia kuandaa wanafunzi wenye ujuzi wa vitendo.

Je, habari hii ilikusaidia?
Sambaza

Maoni 0

Hakuna maoni bado. Kuwa wa kwanza kutoa maoni!

Acha maoni

Barua pepe yako haitachapishwa. Sehemu zenye * ni lazima.