Na Lucy Lyatuu,Dodoma
RAIS , Dkt. Samia Suluhu Hassan, anatarajiwa kuzindua rasmi mji wa serikali eneo la Mtumba, Dodoma Oktoba 30,2026 ambapo ujenzi wa majengo ya ofisi za Wizara na Taasisi za Serikali pamoja na miundombinu ya kisasa, umegharimu bil 700.
Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa, amesema hayo alipozungumza na waandishi wa habari jijini Dodoma kuhusu utekelezaji wa shughuli mbalimbali za Serikali.
Amesema uzinduzi huo, ambao uliahirishwa kufuatia kifo cha mume wa Rais, sasa utafanyika kama ulivyopangwa upya, ukiwa hatua muhimu katika kuimarisha utendaji wa Serikali na hadhi ya Dodoma kama makao makuu ya shughuli za Serikali nchini.
Amesema mradi wa Mji wa Serikali Mtumba umetekelezwa kwa awamu, ambapo awamu ya kwanza ilianza Novemba 28, 2018, kwa ujenzi wa majengo 23 ya ofisi za muda yaliyokamilika Machi 22, 2019.
Ameongeza awamu ya pili ilianza Oktoba 2021, ikilenga kujenga majengo ya kudumu ya Wizara na Taasisi za Serikali pamoja na miundombinu wezeshi.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu, Profesa Palamagamba Kabudi, mradi huo unahusisha majengo ya Wizara 26, Taasisi 11 za Serikali na barabara za lami zenye urefu wa kilomita 57.1 na kwamba miundombinu hiyo inatarajiwa kuwezesha watumishi 18,510 kufanya kazi katika eneo hilo.
Amesema Mji huo umeendelezwa kwa kuzingatia dhana ya mji janja kwa kuweka mifumo ya kisasa ya umeme, maji, mawasiliano na usalama.
Mradi unajumuisha kilomita 42 za miundombinu ya umeme inayopita chini ya ardhi, mifumo ya maji safi na maji taka, TEHAMA pamoja na kamera za ulinzi (CCTV).
Mbali na majengo ya ofisi, Mji wa Serikali Mtumba una barabara za lami, Uwanja wa Mashujaa, kituo cha zimamoto na mifumo ya mifereji ya maji.
Amesema Usanifu wa eneo hilo pia umezingatia utunzaji wa mazingira kupitia mipango inayohusisha matumizi ya nishati mbadala, uvunaji wa maji ya mvua, upandaji miti na uboreshaji wa mandhari, kwa lengo la kujenga mazingira bora na endelevu ya kufanyia kazi.
Uzinduzi huo unatarajiwa kuimarisha uratibu wa shughuli za Serikali kwa kuzikutanisha Wizara na Taasisi mbalimbali katika eneo moja lenye miundombinu ya kisasa.
Maoni 0
Hakuna maoni bado. Kuwa wa kwanza kutoa maoni!