Na Lucy Ngowi
MKURUGENZI Mkuu wa Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma (PPRA), Dennis Simba, amesema ushiriki wa wazabuni katika zabuni za umma unapaswa kuongeza kipato na kutengeneza ajira kwa makundi mbalimbali, yakiwamo vijana na wanawake, ili kukuza uchumi jumuishi nchini.
Simba amesema hayo alipofanya ziara ya kuangalia miradi ya ujenzi inayosimamiwa na Kikundi cha Okoa cha Wazee mkoani Rukwa.
Katika ziara hiyo amesisitiza umuhimu wa wazabuni kutumia fursa za zabuni kujiletea maendeleo na kutoa ajira kwa wengine, huku akieleza kuwa Sheria ya Ununuzi wa Umma ya mwaka 2023 na kanuni zake za mwaka 2024 zinalenga kupanua ushiriki wa makundi mbalimbali katika shughuli za kiuchumi.

Amesema wazabuni wanapaswa kutekeleza miradi kwa ubora na kwa wakati ili kujenga uaminifu na kuongeza nafasi ya kupata zabuni nyingine.
Kauli hiyo inaakisi mafanikio ya Kikundi cha Okoa cha Wazee mkoani Rukwa, ambacho kimepata miradi saba ya ujenzi na matengenezo ya barabara yenye thamani ya zaidi ya Sh. Milioni 270 tangu mwaka 2020.
Mkurugenzi wa kikundi hicho, Stanley Mkulungu, amesema miradi hiyo imekuwa chanzo cha kipato kwa wanachama wenye umri wa miaka 62 hadi 90 na kutoa ajira kwa vijana, ambapo katika baadhi ya maeneo waliweza kuajiri vijana takribani 30.
Amesema kikundi hicho kinatekeleza kazi kupitia Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) na Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA), zikiwamo za kufyeka na kufungua barabara, kusafisha mitaro, kujenga mifereji na makalvati.

Kwa sasa, kikundi hicho kinaendelea na mradi mwingine wa barabara wenye thamani ya takribani Sh. Milioni 63.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Ufundi wa kikundi hicho, Fabian Sanga, amesema wanaendelea kukarabati daraja lililoharibiwa na maji pamoja na kujenga mitaro na makalvati katika barabara za Nyami na Lule, huku mtaro wa Barabara ya Almasi ukiwa umekamilika.
Hata hivyo, amesema uhaba wa fedha ni changamoto inayokwamisha kasi ya utekelezaji wa baadhi ya shughuli, ingawa kikundi kinaendelea kujitahidi kukamilisha miradi kwa wakati.

Kikundi hicho pia kinatarajia kutumia shamba lake la ekari 40 kuimarisha shughuli za kilimo na kuongeza vyanzo vya mapato.
Maoni 0
Hakuna maoni bado. Kuwa wa kwanza kutoa maoni!