Nenda moja kwa moja kwenye maudhui
November 6, 2026
Habari Author 11

Matumizi Ya Mbegu Bora Husaidia Kuzalisha Chakula Cha Kutosha- TOSCI

Na Lucy Lyatuu,Tanga
TAASISI  ya Kuthibiti Ubora wa Mbegu Tanzania (TOSCI) imebainisha kuwa matumizi ya mbegu bora ni hatua muhimu katika kuhakikisha wakulima wanazalisha chakula cha kutosha na chenye ubora.
TOSCI imeendelea kutoa elimu kwa wakulima kuhusu umuhimu wa kutumia mbegu bora,kwa kuwa ni mojawapo ya hatua ya kuonveza uzalisbahi bora wa mazao na kuimarisha usalama wa chakula nchini.
Imesema  kwa mwaka 2026, TOSCI imeweka makadirio ya matumizi ya mbegu bora kufikia tani 120,000, na hadi sasa kiwango kilichofikiwa tayari kimevuka nusu ya lengo hilo. Kwa muda mrefu, taasisi hiyo inalenga matumizi ya mbegu bora kufikia tani 250,000 ifikapo mwaka 2030.
Mtafiti na Mkaguzi Wa Mbegu kutoka TOSCI Aletu Kibalazo amesema hayo katika wiki ya chakula duniani inayoadhimishwa mkoani Tanga katika viwanja vya Usagara.
Amesema usalama wa chakula unaanzia kwenye mbegu bora, akieleza kuwa bila kuhakikisha wakulima wanatumia mbegu zinazokidhi viwango, jitihada za kuongeza uzalishaji wa chakula haziwezi kufikia matokeo yanayotarajiwa.
Aidha amesema Serikali imewekeza katika eneo la mbegu, huku TOSCI ikiendelea na mikakati ya kuhakikisha mbegu bora zinapatikana kwa wingi, zinawafikia wakulima kwa urahisi na zinakuwa na gharama nafuu.
“Mikakati hiyo inazingatia mambo matatu muhimu yanayojulikana kama A3, ambayo ni upatikanaji wa mbegu,  urahisi wa kuzipata) na uwezo wa wakulima kumudu gharama zake,” amesema.
Hata hivyo Kibalazo amesema  upatikanaji wa mbegu pekee hautoshi iwapo wakulima wanashindwa kuzifikia kutokana na umbali au gharama za usafiri ambapo wanaendelea kusajili mawakala wa kusambaza mbegu hadi vijijini ili kurahisisha upatikanaji wake na kupunguza muda na gharama ambazo wakulima hutumia kuzitafuta.
“Kuongezeka kwa upatikanaji wa mbegu bora kunatarajiwa kusaidia wakulima kuzipata kwa urahisi zaidi, huku ongezeko la upatikanaji na matumizi yake likitarajiwa kuchangia kupunguza gharama kulingana na hali ya soko na mahitaji,” amesema.
Ameeleza kuwa maendeleo hayo yanahusishwa na kampeni zinazoendelea za kuhamasisha matumizi ya mbegu bora, huku ushiriki wa TOSCI katika Maonesho ya Siku ya Chakula Duniani ukiwa sehemu ya juhudi za kukutana na wakulima moja kwa moja, kuwapatia elimu na kuwahamasisha kutumia mbegu bora katika shughuli zao za kilimo.
Je, habari hii ilikusaidia?
Sambaza

Maoni 0

Hakuna maoni bado. Kuwa wa kwanza kutoa maoni!

Acha maoni

Barua pepe yako haitachapishwa. Sehemu zenye * ni lazima.