Nenda moja kwa moja kwenye maudhui
November 6, 2026
Habari Lucy Ngowi 11

TMDA Yaonya Matumizi Holela Ya Vijuasumu

Na Lucy Ngowi

MATUMIZI holela ya dawa za vijiuasumu (antibiotics) yanaweza kuchochea usugu wa bakteria, hali inayoweza kufanya maambukizi kuwa magumu kutibika, kuongeza gharama za matibabu na kuhatarisha maisha ya wagonjwa.

Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA) imeeleza kuwa matumizi yasiyo sahihi ya dawa hizo yanaweza kupunguza ufanisi wake, huku bakteria sugu wakiendelea kuongezeka na kusambaa katika jamii.

Ofisa Mwandamizi wa Elimu kwa Umma na Wateja wa TMDA, Edward Bora amesema vijiuasumu ni dawa muhimu katika kutibu magonjwa yanayosababishwa na bakteria, lakini vinapaswa kutumiwa kwa kufuata maelekezo ya wataalamu wa afya.

Habari Picha 14050

Ameeleza kuwa, dawa hizo zinapotumiwa kiholela, bakteria huweza kujenga usugu dhidi ya dawa hizi na kufanya ugonjwa husika kuwa mgumu kutibika. Hali hii inaweza kusababisha uhitaji wa matibabu makubwa yanayoweza kupelekea ongezeko la gharama za matibabu.

Miongoni mwa matumizi yasiyo sahihi ya vijiuasumu ni kununua na kutumia dawa bila maelekezo ya mtaalamu wa afya, kutumia dawa hizo kutibu magonjwa yanayosababishwa na virusi na kutofuata dozi iliyoelekezwa.

Makosa mengine ni kutumia dawa bila kuzingatia mwingiliano wake na dawa au vitu vingine, pamoja na kubadili au kusitisha matibabu bila ushauri wa mtaalamu.

TMDA imewashauri wananchi kutotumia vijiuasumu kiholela, kuhakikisha wanaelewa matumizi ya dawa wanazopewa na kufuata maelekezo ya daktari au mtaalamu wa afya.

Wananchi pia wanatakiwa kutompa mtu mwingine dawa walizoandikiwa na kuuliza wataalamu wa afya wanapokuwa na maswali kuhusu matumizi au madhara ya dawa hizo.

Habari Picha 14051

Vijiuasumu vinapotumiwa kwa usahihi husaidia kutibu maambukizi ya bakteria. Hata hivyo, matumizi yake yasiyofaa yanaweza kuchangia usugu wa bakteria na kuhatarisha uwezo wa dawa hizo kutibu maambukizi kwa ufanisi.

Je, habari hii ilikusaidia?
Sambaza

Maoni 0

Hakuna maoni bado. Kuwa wa kwanza kutoa maoni!

Acha maoni

Barua pepe yako haitachapishwa. Sehemu zenye * ni lazima.