Na Lucy Ngowi
SUMBAWANGA: BENKI ya CRDB imesema inalenga kuwafikia vijana, wakiwamo wenye mahitaji maalum na wahitimu wa mafunzo ya ufundi stadi, kwa kuwapatia fursa za kifedha zitakazowawezesha kujiajiri, kuanzisha biashara na kujitegemea kiuchumi.

Meneja wa Benki ya CRDB tawi la Sumbawanga, Ruhore Masaka, amesema kupitia CRDB Bank Foundation na programu ya iMBEJU, vijana na wanawake wanaweza kupata mitaji wezeshi ya kuanzisha au kuendeleza biashara zao.

Amesema benki hiyo inalenga kuhakikisha vijana wanapata fursa sawa za kifedha bila kujali mazingira wanayotoka au changamoto zinazowakabili, wakiwamo vijana wenye mahitaji maalum.
Masaka amesema programu hiyo ni sehemu ya juhudi za kuwawezesha vijana kutumia uwezo na ujuzi wao kujenga maisha bora kupitia shughuli za kiuchumi.
Kwa upande wake, Meneja wa Mahusiano na Taasisi za Serikali wa CRDB, Paskalina Diu, amesema benki hiyo imevutiwa na mafunzo ya ufundi stadi yanayotolewa na Chuo cha Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA), kutokana na mchango wake katika kuwawezesha vijana kujiajiri na kuajiriwa.

Diu amesema kupitia kliniki ya CRDB Bank Foundation, benki hiyo itaangalia namna ya kuwasaidia vijana wanaopata mafunzo hayo ili waweze kutumia ujuzi wao kuanzisha na kuendeleza biashara.

Amesema CRDB pia inatoa elimu ya fedha na huduma maalum kwa wanafunzi, ikiwamo Boom Advance, inayowawezesha wanafunzi wa vyuo kupata hadi asilimia 80 ya fedha za kujikimu wanazosubiri kutoka Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB), kwa kuzingatia masharti ya huduma hiyo.

Diu ameyasema hayo wakati wa Maonesho ya Wiki ya Vijana Kitaifa mjini Sumbawanga, yanayofanyika chini ya kaulimbiu, “Tanzania ni Yetu Sote, Tushikamane kwa Pamoja Kuleta Maendeleo.”
Maoni 0
Hakuna maoni bado. Kuwa wa kwanza kutoa maoni!