Nenda moja kwa moja kwenye maudhui
November 6, 2026
Habari Lucy Ngowi 21

TBA Yashika Nafasi Ya Pili Maonesho Ya Madin

Na Lucy Ngowi
GEITA: WAKALA wa Majengo Tanzania (TBA) umeibuka mshindi wa pili katika kundi la taasisi za umma zilizoshiriki Maonesho ya Tisa ya Kitaifa ya Teknolojia ya Madini yanayoendelea Geita, mafanikio ambayo umeeleza kuwa yamechangiwa na ushirikiano wa wadau waliotembelea banda lake.
Akizungumza katika maonesho hayo, Meneja Mawasiliano na Masoko wa TBA, Adam Mwingira, amesema tuzo hiyo ni ya wadau wote walioshiriki kutembelea banda la taasisi hiyo na kufuatilia shughuli zake, huku ikionyesha mwitikio wa wananchi na wawekezaji kwa huduma na fursa zinazotolewa na TBA.
Habari Picha 13964
Amesema kupitia maonesho hayo, TBA imekuwa ikitangaza fursa za uwekezaji katika maeneo mbalimbali nchini, ikiwemo maeneo mawili yaliyopo Geita ambayo yameandaliwa kwa ajili ya uwekezaji kupitia ubia kati ya Serikali na sekta binafsi (PPP).
“Tunayo maeneo mawili Geita yaliyo tayari kwa uwekezaji, ambayo ni Misheni Kota yenye ukubwa wa takribani mita za mraba 10,600 na eneo la Msikitinii,” amesema.
Kwa mujibu wa Mwingira, TBA pia ina maeneo mengine 38 katika Tanzania Bara ambayo yanatangazwa kwa wawekezaji wanaotaka kuwekeza katika miradi ya ujenzi na makazi.
Amesema katika eneo la Bishota, Geita, TBA inapanga kujenga majengo ya makazi yenye ghorofa takribani sita na jumla ya nyumba 12, zikiwa na vyumba vya kulala vya aina mbalimbali, ikiwemo vyumba vitatu, viwili na kimoja.
Habari Picha 13966
Mwingira amesema TBA pia imekuwa ikitekeleza miradi mbalimbali ya ujenzi kwa Serikali na wananchi, ikiwemo nyumba za viongozi, hospitali na makazi ya watumishi wa umma pamoja na wananchi wengine.
Amesema miongoni mwa miradi hiyo ni Hospitali ya Chato na Hospitali ya Geita, huku TBA pia ikiwa mshauri wa Serikali katika miradi ya majengo, ikiwemo jengo la Serikali Chamwino, Dodoma, ambako imehusika katika usanifu na usimamizi wa ujenzi.
Aidha, amesema TBA imeendelea na ujenzi wa nyumba za makazi katika maeneo mbalimbali, ikiwemo Magomeni, Dar es Salaam, ambako awamu ya kwanza imekamilika na awamu nyingine inaendelea.
Mwingira amewashukuru wadau waliotembelea banda la TBA na kuitaja tuzo hiyo kuwa kichocheo cha kuendelea kutoa huduma na kutangaza fursa za uwekezaji katika sekta ya ujenzi nchini.
Je, habari hii ilikusaidia?
Sambaza

Maoni 0

Hakuna maoni bado. Kuwa wa kwanza kutoa maoni!

Acha maoni

Barua pepe yako haitachapishwa. Sehemu zenye * ni lazima.