Na Lucy Ngowi
GEITA: ZAIDI ya vijana 1,500 nchini wamesajiliwa katika mpango unaolenga kuwawezesha kupata ujuzi, ajira na kujiajiri, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuwajengea uwezo wa kujitegemea kiuchumi.
Akizungumza katika Maonesho ya Tisa ya Kitaifa ya Teknolojia ya Madini yanayoendelea Geita, Balozi wa Amani Tanzania, Mess Mbura, amesema mpango huo unalenga kuhakikisha vijana wanapata fursa za kiuchumi na kushiriki kikamilifu katika maendeleo ya Taifa.
Amesema kuwa Balozi wa Amani kunaenda sambamba na kusaidia vijana kupata ajira na kuwaunganisha na waajiri, huku waajiri wakipewa elimu na mbinu zinazoweza kuwasaidia kufikia mafanikio katika shughuli zao.
“Lengo kuu ni kuwasaidia vijana, kwa sababu huwezi kuwa Balozi wa Amani bila kusaidia vijana kupata ajira na fursa za kiuchumi,” amesema.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Youth Foundation Tanzania, Yazidu Mtika, amesema taasisi hiyo inalenga kuwawezesha vijana kuwa na uwezo wa kujitegemea kiuchumi kupitia mafunzo, elimu na mazingira wezeshi ya kutekeleza miradi yao.
Amesema taasisi hiyo inatekeleza na kuunga mkono miradi katika sekta mbalimbali, ikiwemo madini, kilimo, uvuvi, teknolojia na ufugaji.
“Tunawasaidia vijana kuwa na uwezo wa kujitegemea kiuchumi kwa kuwapatia mafunzo, elimu na kuwawezesha kupata mazingira mazuri ya kutekeleza miradi yao,” amesema.
Mtika amesema taasisi hiyo pia inakaribisha vijana kutoka maeneo mbalimbali kushiriki katika programu zake za uwezeshaji.
Aliongeza kuwa Oktoba nne, mwaka huu 2026 watafanya mafunzo ya uchumi kwa vijana wa Mkoa wa Geita kwa lengo la kuwajengea uwezo wa kutumia fursa zilizopo katika maeneo yao.
Maoni 0
Hakuna maoni bado. Kuwa wa kwanza kutoa maoni!