Na Mwandishi Wetu
WINDHOEK, NAMIBIA: AFRIKA imehimizwa kuacha kutegemea teknolojia zinazotengenezwa nje ya bara hilo na badala yake kutumia uwezo wa wanasayansi wake, vijana na maarifa ya asili kubuni teknolojia zinazokidhi mahitaji ya Waafrika.
Waziri Mkuu wa Namibia, Dkt. Tjitunga Ngurare, ametoa wito huo wakati akifungua Jukwaa la Washirika wa Mpango wa Kuimarisha Taasisi za Ufadhili wa Utafiti Afrika (SGCI) mjini Windhoek, Septemba 30, 2026.
Dkt. Ngurare amewataka wanasayansi wa Afrika kuchunguza maarifa ya asili na kujiuliza kama baadhi yake yanaweza kutoa mwanga wa kubuni teknolojia mpya zinazoweza kutengenezwa na kutumika barani humo.
Ametumia simulizi za Kiafrika kuhusu kusafiri usiku na kuwasiliana kutoka maeneo ya mbali kama mifano ya masuala ambayo, licha ya kuonekana kuwa si ya kawaida, yanaweza kuibua maswali ya kisayansi na kuchochea utafiti.
“Ikiwa nimekosea, mababu zetu watanısamehe,” amesema, akisisitiza umuhimu wa wanasayansi kuwa tayari kuuliza maswali na kuchunguza mawazo ambayo yanaweza kupuuzwa.
Hata hivyo, Dkt Ngurare hakudai kuwa simulizi hizo zimethibitishwa kisayansi kuwa teknolojia za mawasiliano, bali alizitumia kuhamasisha watafiti kufikiria zaidi ya yaliyozoeleka na kuchunguza maarifa ambayo huenda yakawa na manufaa baada ya kufanyiwa utafiti.
Amehoji pia kwa nini sehemu kubwa ya programu na vifaa vya kompyuta vinavyotumiwa Afrika hutengenezwa nje ya bara hilo, licha ya kuwepo kwa wanasayansi, wahandisi na vijana wenye uwezo wa kubuni.
“Samsung ya Afrika itakuja lini? Apple ya Afrika itakuja lini?” amehoji.
Amezitaka serikali za Afrika kusikiliza watafiti, kutumia utaalamu wao na kuwapa vijana nafasi ya kukuza mawazo mapya, akisema utafiti unapaswa kusaidia kupata majibu ya changamoto za chakula, afya, nishati, maji, mabadiliko ya tabianchi na teknolojia za kidijitali.
Tanzania iliwakilishwa katika ufunguzi huo na Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH), Dkt. Amos Nungu, aliyetoa shukrani kwa niaba ya washiriki wa SGCI.
Dk Nungu amesema taasisi zinazofadhili utafiti zina wajibu wa kusaidia tafiti zinazojibu mahitaji ya jamii, akisisitiza umuhimu wa kuimarisha taasisi na ushirikiano ili maarifa yanayozalishwa yageuke kuwa sera bora, suluhisho zinazotumika na maisha bora kwa wananchi.
Maoni 0
Hakuna maoni bado. Kuwa wa kwanza kutoa maoni!