Nenda moja kwa moja kwenye maudhui
November 6, 2026
Habari Lucy Ngowi 18

NBS: Takwimu Sahihi Msingi Wa Uchumi Wa Madini

Na Lucy Ngowi

GEITA: UCHUMI wa Tanzania umeendelea kukua baada ya kufikia asilimia 6.1 katika robo ya kwanza ya mwaka 2026, kutoka asilimia 5.9 katika kipindi kama hicho mwaka 2025, huku sekta ya madini ikichangia asilimia 10.3 ya Pato la Taifa mwaka 2025.

Takwimu hizo zimetolewa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) Mkoa wa Geita wakati wa Maonyesho ya Teknolojia ya Madini yanayoendelea katika Viwanja vya Dkt. Samia Suluhu Hassan mkoani Geita.

Meneja Takwimu wa NBS Mkoa wa Geita, Khalid Msabaha, amesema takwimu rasmi ni msingi muhimu wa kufanya maamuzi sahihi katika shughuli za kiuchumi, hasa katika sekta ya madini na mnyororo wake wa thamani.

Amesema NBS imeshiriki maonyesho hayo kwa lengo la kuwaelimisha wadau kuhusu umuhimu wa kutumia takwimu rasmi katika kupanga uzalishaji, uwekezaji na shughuli nyingine za maendeleo.

“Takwimu siyo namba zinazokusanywa kwa ajili ya kumbukumbu pekee, bali ni nyenzo ya kuelewa mwenendo wa uchumi na kufanya maamuzi yanayozingatia uhalisia,” amesema.

Kwa mujibu wa Msabaha, umuhimu wa takwimu unaonekana zaidi Geita ambako shughuli za madini ni sehemu muhimu ya uchumi na huchochea biashara, huduma, usafirishaji, ajira na shughuli nyingine zinazounda mnyororo wa thamani.

Amesema serikali, wafanyabiashara, wawekezaji na wadau wengine wanapaswa kutumia taarifa sahihi na zinazopatikana kwa wakati katika kupanga shughuli zao.

Msabaha amesema matumizi ya takwimu rasmi ni muhimu pia katika kufanikisha malengo ya maendeleo ya taifa kupitia Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050.

Je, habari hii ilikusaidia?
Sambaza

Maoni 0

Hakuna maoni bado. Kuwa wa kwanza kutoa maoni!

Acha maoni

Barua pepe yako haitachapishwa. Sehemu zenye * ni lazima.