Na Lucy Ngowi
GEITA: ALIYEKUWA Mkuu wa Wilaya ya Chato, Luis Bura, amewataka wananchi kushirikiana na taasisi za nishati kulinda miundombinu ya umeme na kutoa taarifa mapema kuhusu changamoto zinazoweza kuhatarisha huduma, huku akihimiza matumizi ya nishati safi kwa ajili ya kulinda mazingira.
Bura ametoa rai hiyo baada ya kutembelea banda la Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) katika Maonyesho ya Tisa ya Teknolojia ya Madini Kitaifa yanayofanyika mkoani Geita.
Amesema wananchi wana nafasi kubwa katika kulinda miundombinu ya umeme kwa kutoa taarifa kuhusu changamoto wanazoziona katika maeneo yao, ikiwemo nguzo zilizo katika hatari ya kuanguka na miundombinu mingine inayoweza kuathiri upatikanaji wa huduma.
“Ni muhimu wananchi wapate elimu ya matumizi sahihi ya nishati na utunzaji wa miundombinu ya umeme, kwa sababu wao ndio wanaoishi karibu na miundombinu hiyo na wanaweza kutoa taarifa mapema,” amesema.
Bura pia ameipongeza TANESCO kwa kutumia teknolojia na mifumo ya mawasiliano katika kuboresha huduma kwa wananchi, akisema hatua hiyo imerahisisha utoaji wa taarifa na utatuzi wa changamoto za umeme.

Amesema katika baadhi ya maeneo, wananchi wamekuwa wakipata huduma kwa haraka kupitia vikundi vya mawasiliano vinavyowaunganisha na watendaji wa TANESCO, badala ya kufika ofisini kufuatilia changamoto.
Katika hatua nyingine, Bura amesisitiza matumizi ya nishati safi, akisema utegemezi mkubwa wa nishati inayochangia ukataji wa miti unaweza kuongeza uharibifu wa mazingira na kuathiri mustakabali wa nchi.
Amesema Serikali imekuwa ikihamasisha matumizi ya nishati safi na kuwataka wananchi kutumia fursa zinazotolewa kupitia TANESCO na REA, ikiwemo teknolojia za kisasa za kupikia.
Kwa upande wake, Ofisa Uhusiano na Huduma kwa Wateja Mkoa wa Geita, Lucas Swere, amesema TANESCO imekuwa ikitoa elimu kwa wananchi kuhusu umuhimu wa kuachana na matumizi ya nishati chafu na kuhamia kwenye nishati safi.
Amesema shirika hilo limekuja na majiko ya teknolojia mbalimbali yanayolenga kurahisisha shughuli za upishi na kupunguza matumizi ya nishati zinazochafua mazingira.
Ametaja baadhi ya teknolojia hizo kuwa ni majiko yanayotumia mfumo wa pressure cooker na yale ya induction.
Swere amewataka wananchi wanaotembelea maonyesho hayo kufika katika banda la TANESCO kupata elimu kuhusu matumizi ya nishati safi, utunzaji wa mazingira na namna teknolojia hizo zinavyoweza kurahisisha shughuli za kila siku.
Amesema matumizi ya nishati safi yanaweza kusaidia kupunguza utegemezi wa nishati zinazochangia ukataji wa miti, huku wananchi wakinufaika na teknolojia zinazorahisisha maisha yao.
Maoni 0
Hakuna maoni bado. Kuwa wa kwanza kutoa maoni!