Na Lucy Ngowi
GEITA: MCHIMBAJI mmoja mkoani Geita aliyefikia hatua ya kuiomba Serikali ifute leseni zake kutokana na kushindwa kuendeleza shughuli za uchimbaji, amerejea mgodini baada ya kupata mwekezaji kutoka China na kuingia naye katika ushirikiano.
Akieleza safari hiyo, Emmanuel Francis Jirab kutoka Kampuni ya Yi Xing Kuangye Mining Co. Ltd, amesema mchimbaji huyo alikumbwa na ukosefu wa mtaji pamoja na changamoto ya maji kujaa katika maduara ya uchimbaji, hali iliyosababisha shughuli kusimama kwa muda.
Amesema kutokana na kushindwa kuziendeleza leseni zake, mchimbaji huyo alianza kuziona kama mzigo na hatimaye akaiandikia Wizara ya Madini akiomba zifutwe rasmi.

Hata hivyo, wakati akisubiri mchakato wa maombi hayo, wawekezaji kutoka China walifika katika eneo lake la uchimbaji, wakafanya ziara na kuonyesha nia ya kuingia naye katika ushirikiano.
“Wawekezaji walipokuja, walikuja wenyewe nyumbani, mimi sikuwatafuta. Wakatembelea na kukubali kwamba tutafanya nao uchimbaji,” amesema Jirab.
Baada ya kufikia makubaliano, mchimbaji huyo alirejea Wizara ya Madini ili kuzuia mchakato wa kufuta leseni zake na kuendelea na shughuli za uchimbaji.
Jirab amesema ushirikiano huo umewezesha shughuli kuanza tena katika maeneo yaliyokuwa yamesimama, na mchimbaji huyo kuanza kupata mafanikio ya kifedha baada ya kipindi cha changamoto.
Amesema mafanikio hayo yamemwezesha kugharamia mahitaji ya familia yake, ikiwemo elimu ya mtoto wake anayesoma nje ya nchi.
Maoni 0
Hakuna maoni bado. Kuwa wa kwanza kutoa maoni!