Nenda moja kwa moja kwenye maudhui
November 6, 2026
Habari Lucy Ngowi 16

Wananchi Waonywa Kutumia Taasisi Za Fedha Zisizo Na Leseni

Na Lucy Ngowi

GEITA: WANANCHI, hususan wachimbaji wa madini na wakazi wa maeneo ya uchimbaji, wametakiwa kuwa makini na taasisi zinazotoa huduma za fedha bila leseni ya Benki Kuu ya Tanzania (BoT), wakielezwa kuwa kutumia taasisi zilizoidhinishwa kunawawezesha kupata ulinzi na msaada wanapokumbana na migogoro ya kifedha.

Wito huo umetolewa na Ramadhani Myonga, Ofisa Sheria Mwandamizi kutoka Kurugenzi ya Ustawi na Huduma Jumuishi za Fedha, Kitengo cha Kumlinda Mtumiaji wa Huduma za Fedha, wakati akizungumza katika Maonesho ya Tisa ya Kitaifa ya Teknolojia ya Madini, yaliyofanyika katika Viwanja vya Dkt. Samia Suluhu Hassan, Geita.

Myonga amesema elimu hiyo inalenga kuwawezesha wananchi kutumia huduma za fedha kwa usalama na kuchangia katika juhudi za kufikia malengo ya maendeleo, ikiwamo Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050.

Amesema wananchi wanapaswa kuhakiki kwanza kama taasisi wanayotaka kutumia huduma zake ina leseni au idhini halali ya BoT, kwa kuwa kufanya hivyo kunawapa fursa ya kupata ulinzi wa mifumo rasmi ya udhibiti wa huduma za fedha.

“Ni muhimu mwananchi akahakikisha anatumia huduma ya taasisi ya fedha iliyosajiliwa na Benki Kuu ya Tanzania kwa sababu anapopata changamoto anaweza kupata ulinzi na kutumia mifumo rasmi ya kuwasilisha malalamiko,” amesema.

Amesema changamoto zinazoweza kujitokeza ni pamoja na kuongezewa riba au gharama bila kufuata taratibu, kunyimwa huduma au kutotendewa kwa mujibu wa makubaliano.

Pia amesema, BoT imeweka mfumo wa kidijitali ‘Sema na BOT’ unaomwezesha mwananchi kuwasilisha malalamiko kuhusu huduma za kifedha.

Amesema mwananchi ambaye amewasilisha malalamiko katika taasisi husika na hajapata majibu ndani ya siku nne anaweza kutumia mfumo huo kupitia tovuti ya BoT.

Myonga alisema Microfinance Act, 2018, kupitia Kifungu cha 16(1), inakataza kufanya biashara ya huduma ndogo za fedha bila leseni, huku Kifungu cha 16(2) kikieleza adhabu kwa wanaokiuka masharti hayo.

Amesisitiza wananchi kutumia taasisi zilizoidhinishwa ili kuepuka hasara na kupata ulinzi wa kisheria wanapokumbana na migogoro ya kifedha.

Je, habari hii ilikusaidia?
Sambaza

Maoni 0

Hakuna maoni bado. Kuwa wa kwanza kutoa maoni!

Acha maoni

Barua pepe yako haitachapishwa. Sehemu zenye * ni lazima.