Na Mwandishi Wetu
DODOMA: SERIKALI imeongeza nguvu katika hatua za kukabiliana na changamoto ya wanyamapori wakali na waharibifu, hasa Tembo wanaovamia makazi na mazao ya wananchi.
Mbinu zinazotumika ni pamoja na uanzishaji wa vituo vya Askari wa wanyamapori karibu na maeneo ya hifadhi ili kuhakikisha mwitikio wa haraka kwa tukio lolote linalohusisha wanyama hao.

Waziri Mkuu, Dkt. Mwigulu Nchemba, ametoa ufafanuzi huo Bungeni Jijini Dodoma wakati akijibu maswali ya Wabunge katika Mkutano wa 3 wa Bunge la 13.
Amesema Wizara ya Maliasili na Utalii inatekeleza mpango wa kuanzisha vituo hivyo katika kila eneo lililo hatarini, ili kupunguza athari zinazotokana na wanyamapori hao kwa wananchi.
“Serikali pia imekuja na mbinu mpya za kuwafukuza wanyama hawa, mojawapo ikiwa ni kutumia ndege za nyuki pindi wanyama wanapobainika kuelekea maeneo ya wananchi,” amesema Dkt. Nchemba.
Aidha, Waziri Mkuu ameongeza kuwa Wizara itazidisha idadi ya Askari wa wanyamapori katika maeneo yenye upungufu wa walinzi ili kuhakikisha mwitikio wa haraka na ufanisi, sambamba na juhudi za kupambana na ujangili.
Dkt. Nchemba pia alifafanua kuwa Tanzania ni mwanachama wa mikataba ya kimataifa inayolinda wanyamapori, ikiwemo Tembo, kuhakikisha hawaharibiki, hawauwawi kiholela, na mazao yao yasihamishwe bila utaratibu.

Hii ni hatua muhimu katika kuhifadhi urithi wa wanyamapori na kulinda maslahi ya wananchi wanaoishi karibu na hifadhi.
Serikali inasisitiza kuwa mikakati hii ya kuimarisha ulinzi wa wanyamapori itasaidia kupunguza migongano kati ya binadamu na wanyama, huku ikihakikisha hifadhi za wanyamapori zinaendelea kuendelezwa kwa njia endelevu.


