Na Lucy Ngowi
KWA mara ya kwanza, Mamlaka ya Afya ya Mimea na Viuatilifu Tanzania (TPHPA) imeanzisha programu maalum ya kufuatilia masalia ya viuatilifu kwenye mazao yanayoingia katika masoko ya ndani, hatua inayolenga kulinda afya ya walaji.
Akizungumza na vyombo vya habari kuhusu mafanikio ya mamlaka hiyo kwa kipindi cha mwaka 2023/2024 hadi 2025/2026, Mkurugenzi Mkuu wa TPHPA, Profesa Joseph Ndunguru, amesema kuwa utekelezaji wa programu hiyo tayari umefanyika katika mikoa 10 ya Tanzania Bara pamoja na Zanzibar (Unguja na Pemba).
Aidha kazi ya uchukuaji sampuli inaendelea katika mikoa mingine.
Katika kuimarisha shughuli za udhibiti na ukaguzi, TPHPA imefanikiwa kuwajengea uwezo wakaguzi 82 wa mazao na viuatilifu kupitia mafunzo maalum, ili kuboresha utendaji wao mipakani na katika kanda mbalimbali.
Sambamba na hilo, mamlaka hiyo imetoa mafunzo kwa vijana wa programu ya BBT 365, ambapo vijana 118 kutoka Chinangali na 147 kutoka Ndogowe walifundishwa kuhusu udhibiti wa visumbufu vya mimea pamoja na matumizi sahihi na salama ya viuatilifu.
Kwa upande wa usalama wa viuatilifu, TPHPA imefanya uchambuzi wa viuatilifu hatarishi vinavyotumika nchini na kubaini uwepo wa viambata amilifu hatarishi 18.
Kutokana na matokeo hayo, jumla ya viuatilifu 130 vimeondolewa sokoni.
Aidha, kwa sasa mamlaka hiyo inaendelea kufanya tathmini ya kiasi cha viuatilifu chakavu kilichopo nchini, kwa lengo la kuratibu utaratibu sahihi wa kuviteketeza kwa kushirikiana na Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC).

