Na Lucy Ngowi
DODOMA: KATIBU Mkuu wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania (TUCTA), Henry Mkunda, amesema shirikisho hilo litaendelea kuhimiza vyama vya wafanyakazi nchini kuweka kipaumbele kwa wanawake kwa kuhakikisha katiba za vyama hivyo zinatenga nafasi za uongozi.
Mkunda, ambaye pia ni Katibu Mkuu wa Chama cha Wafanyakazi wa Serikali na Afya Tanzania (TUGHE), ametoa kauli hiyo leo Machi 7, 2025 wakati wa maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani yaliyoandaliwa na shirikisho hilo, yaliyofanyika mkoani Dodoma.
Amesema shirikisho hilo linaendelea kusisitiza ushiriki wa wanawake katika vyama vya wafanyakazi kuanzia ngazi ya juu hadi matawi, ili kuwapa nafasi ya kushiriki kikamilifu katika maamuzi na uongozi.

Mkunda ametaja pia vyama vipya vinavyoendelea kujiunga na shirikisho hilo,, ikiwemo Chama cha Wafanyakazi wa Vyombo vya Habari Tanzania (JOWUTA), kuwa vitazingatia usawa wa kijinsia katika katiba na mifumo yake ya uongozi.
“Katika vyama vya wafanyakazi tuna kamati kuanzia ngazi ya juu hadi kwenye matawi, na tunahakikisha wanawake wanapata nafasi ya kushiriki na kuongoza,” amesema Mkunda.

Aidha, ameiomba Serikali kuendelea kuboresha sera na mazingira ya kazi yanayowahusu wanawake, hususan wale wanaosafiri kwenda kufanya kazi nje ya nchi.
Amesema shirikisho hilo limeanza kutekeleza programu mbalimbali za kuwawezesha wafanyakazi wanaokwenda kufanya kazi nje ya Tanzania, kupitia ushirikiano wa mashirikisho ya wafanyakazi katika nchi za Kiarabu, ili kuhakikisha wanapata ulinzi na msaada wa vyama vya wafanyakazi wanapofika huko.
Mkunda amesisitiza kuwa wanawake wana mchango mkubwa katika maendeleo ya jamii, akieleza kuwa mbali na kuwa viongozi ndani ya familia na wahusika wakuu wa malezi, pia wanachangia katika shughuli za kiuchumi na za kiimani.

Ameongeza kuwa kuwezeshwa kwa wanawake katika sekta ya ajira na uongozi wa vyama vya wafanyakazi ni hatua muhimu katika kuimarisha usawa na maendeleo ya kijamii nchini.



