Na Lucy Ngowi
DODOMA: MBUNGE wa Mbeya Mjini, Patrick Mwalunenge, amesema changamoto kubwa katika utekelezaji wa mipango ya maendeleo nchini ni uhaba wa rasilimali watu wenye uelewa na fikra za kibiashara, hususan katika ngazi za halmashauri.
Ameeleza hayo bungeni jijini Dodoma wakati akichangia mipango ya utekelezaji ya Dira ya Taifa 2050.
Mwalunenge amesema licha ya mipango mizuri inayowasilishwa na Serikali, utekelezaji wake umekuwa dhaifu kwa sababu watendaji waliopo chini hawana uwezo wala mtazamo wa kibiashara, ilhali mpango huo kwa kiasi kikubwa unajikita kwenye dhana ya uchumi na biashara.
Amesema maoni yake yamejikita zaidi katika sekta ya uzalishaji, hususan kilimo ambacho kinaajiri kati ya asilimia 75 hadi 80 ya Watanzania.
Amekumbusha kuwa Serikali imejiwekea lengo la kufanya sekta ya kilimo kuchangia angalau asilimia 10 ya Pato la Taifa ifikapo mwaka 2030, akisisitiza kuwa lengo hilo halitafikiwa bila dhamira ya dhati katika utekelezaji.
Mwalunenge amesema sekta ya kilimo ndiyo nguzo kuu ya ajira nchini, lakini bado bodi za mazao ya kimkakati kama pamba, korosho, kahawa, kokoa, alizeti na ufuta hazijawezeshwa kifedha.
Ametolewa mfano Bodi ya Pamba ambayo kwa miaka mitano imekuwa ikihangaika kufikia uzalishaji wa tani laki tano, huku zaidi ya watu milioni 15 wa Kanda ya Ziwa wakitegemea zao hilo.
Aliongeza kuwa Tanzania inaendelea kutumia fedha nyingi kuagiza nguo kutoka nje, ilhali ina uzalishaji wa pamba, lakini ukosefu wa mtaji umezuia kufikiwa kwa uzalishaji unaohitajika kuanzisha viwanda vya nguo kuanzia ngazi ya nyuzi hadi bidhaa kamili.
Mwalunenge ameishauri Wizara ya Fedha kuziwezesha bodi za mazao kwa mitaji na kutoa dhamana maalum kwa uwekezaji wa kilimo.
Amesema mafanikio ya zao la korosho, ambapo uzalishaji umeongezeka na wakulima kupata zaidi ya Sh. Trilioni 1.5, ni ushahidi kuwa uwekezaji wa makusudi katika kilimo unaweza kutatua changamoto nyingi ikiwemo ajira, mapato na hata bima ya afya kwa wakulima.
Aidha, amesisitiza umuhimu wa Serikali kuweka mkakati mahsusi wa kutafuta masoko ya mazao nje ya nchi kwa kushirikisha balozi zake.

