Na Mwandishi wetu, Dodoma
BODI ya Ununuzi na Ugavi kwa Umma Tanzania (PSPTB) imetangaza rasmi matokeo ya mitihani ya 32 ya kitaaluma, na kuwahimiza watahiniwa waliokosa alama za kufaulu kujisajili upya na kurudia masomo yao kwa ajili ya mitihani itakayofanyika Mei 2026.
Mkurugenzi Mtendaji wa PSPTB, Godfred Mbanyi, amesema kuwa PSPTB ni taasisi ya Umma iliyoanzishwa kwa mujibu wa Sheria ya Bunge namba 23 ya mwaka 2007, ikiwa na jukumu la kuendesha mafunzo na mitihani ya kitaaluma katika fani ya Ununuzi na Ugavi katika ngazi mbalimbali.
Mbanyi amesisitiza kuwa PSPTB haitasita kuchukua hatua kali dhidi ya yeyote atakayekiuka kanuni na taratibu za mitihani, ikiwemo kufutiwa matokeo, kusimamishwa kushiriki mitihani kwa vipindi vitatu mfululizo, kutozwa faini au hata kifungo cha jela, ili kulinda maadili na uadilifu katika tasnia ya Ununuzi na Ugavi nchini.

Aidha Bodi hiyo imetoa pongezi kwa watahiniwa waliofaulu na kutoa onyo kali kwa wanaojihusisha na vitendo vya ukiukwaji wa kanuni na taratibu za mitihani.
Mbanyi, amesema kuwa PSPTB ni taasisi ya Umma iliyoanzishwa kwa mujibu wa Sheria ya Bunge namba 23 ya mwaka 2007, ikiwa na jukumu la kuendesha mafunzo na mitihani ya kitaaluma katika fani ya Ununuzi na Ugavi katika ngazi mbalimbali.

Ameeleza kuwa uendeshaji wa mitihani hiyo ni utekelezaji wa matakwa ya sheria, mtaala pamoja na maombi ya muda mrefu kutoka kwa wadau wa fani hiyo.
Amesema jumla ya watahiniwa 1,291 walidahiliwa kushiriki mitihani ya 32, ambapo watahiniwa 1,223 walifanya mitihani hiyo huku watahiniwa 68 wakishindwa kuhudhuria kwa sababu mbalimbali.
Amefafanua kuwa kati ya watahiniwa waliofanya mitihani, watahiniwa 595 sawa na asilimia 48.7 wamefaulu huku akisema watahiniwa 589 sawa na asilimia 48.2 watalazimika kurudia masomo yao ambapo watahiniwa 39 sawa na asilimia 3.2 wamefeli na kuanza upya masomo yao katika ngazi husika.
Mbanyi amesema PSPTB inatoa pongezi za dhati kwa watahiniwa wote waliofaulu mitihani yao katika ngazi zote, pamoja na wale waliopata sifa za kutunukiwa Vyeti vya Professional Diploma, Graduate Professional na CPSP.
Aidha amewapongeza wahadhiri na wakufunzi kutoka vyuo na vituo mbalimbali vya mafunzo kwa mchango wao mkubwa katika kuwaandaa watahiniwa.
Mbanyi amesema PSPTB imebaini na kuwakamata watahiniwa wawili wa ngazi ya CPSP wakijihusisha na vitendo vya ukiukwaji wa taratibu za mitihani, baada ya kukutwa wakiwa na karatasi ambazo inasadikika zililenga kuwasaidia kujibu mitihani yao.

Alieleza kuwa Bodi ya Wakurugenzi imeielekeza Kamati ya Usajili na Nidhamu kushughulikia suala hilo, na endapo wahusika watapatikana na hatia, hatua kali zitachukuliwa kwa mujibu wa kanuni zilizopo. Kwa sasa, matokeo ya watahiniwa hao yamezuiliwa wakisubiri kusikilizwa.
Ametoa wito kwa wazazi, wadhamini na waajiri kuwasaidia watahiniwa kwa kuwalipia ada za maandalizi na mitihani, hatua itakayosaidia kuongeza idadi ya wataalam wenye ujuzi na maarifa katika sekta ya Ununuzi na Ugavi.

