Na Lucy Ngowi
DODOMA: MBUNGE wa Jimbo la Monduli, Isack Joseph, amesema anazitambua changamoto zinazowakabili wananchi wa jimbo lake, huku akitaja changamoto kubwa zaidi kuwa ni upatikanaji wa maji.
Akizungumza leo, Novemba 11, 2025, nje ya Viwanja vya Bunge katika mkutano wa kwanza wa Bunge la 13 jijini Dodoma, Joseph amesema anayo dhamira ya dhati ya kusimama kidete kuwatumikia wananchi wa Monduli na kuhakikisha changamoto zao zinatafutiwa ufumbuzi wa kudumu.

“Monduli naijua vizuri. Nimewahi kuwa Mwenyekiti wa Halmashauri, hivyo najua nini kinachowakabili wananchi wangu. Nawaahidi nitakuwa mwakilishi mzuri na nitasimama imara kuzungumzia masuala ya maji, elimu, barabara na afya,” amesema.
Mbunge huyo ameshukuru wananchi wa Monduli kwa kumpa imani na fursa ya kuwawakilisha bungeni, akiahidi kutumika kwa uadilifu na uwajibikaji.
Kadhalika, ametumia nafasi hiyo kumpongeza Rais Samia Suluhu Hassan na Spika wa Bunge, Azzan Zungu, akisema ataunga mkono juhudi zao katika kuwaletea Watanzania maendeleo.
“Wananchi wa Monduli wategemee mambo mazuri. Tutashirikiana na Serikali kuhakikisha changamoto zinazowakabili zinatatuliwa kwa wakati,” alisema Joseph.

