Na Mwandishi Wetu
SHINYANGA: CHAMA cha Ukombozi wa Umma (CHAUMMA) kimesema sera yake katika sekta ya rasilimali ni kuwamilikisha wazawa ili wanufaike na utajiri wa nchi.
Akizungumza na wananchi wa Bulige, Jimbo la Msalala, mgombea urais wa CHAUMMA Salum Mwalim amesema inasikitisha kuona mikoa yenye madini na mazao ya kibiashara ikiendelea kuwa maskini.
Mwalim amesema, licha ya uwepo wa migodi mikubwa ya dhahabu kama Bulyanhulu na Buzwagi, wananchi hawana miundombinu bora ya barabara, maji safi na salama, wala madaktari na wauguzi wa kutosha katika kituo cha afya kilichopo.
“Haya maisha magumu hamyaoni, ndugu zangu wa Msalala? Pia hamjui yamesababishwa na nani?” ameuliza Mwalim.
Ameongeza kuwa mgodi wa Buzwagi umefungwa huku wageni waliokuwa wakichukua dhahabu wakiendelea kunufaika, lakini wananchi wakiwa hawajafaidika chochote.
Mwalim amewataka wakazi wa Msalala kuamka Oktoba 29, mwaka huu 2025 na kuipigia kura CHAUMMA, chama kitakachotetea rasilimali zao.
“Mkiendelea na msimamo wenu wa hyena hyena, tieni tieni kwa CCM, huduma za afya mtakuwa mkizisikia kwa wenzenu; barabara nzuri na maji hivyo hivyo.
“Msalala, nendeni mkapige kura ya hasira, ikataeni CCM kwa sababu mnayo sababu. Nendeni mkanikabidhi nchi hii ili tufanye maendeleo inawezekana kabisa.” amesema.

