Na Mwandishi Wetu
TABORA: MGOMBEA urais kupitia Chama cha Ukombozi wa Umma (CHAUMMA), Salum Mwalim, amesema hataki wabunge ‘machawa’ bali wabunge madhubuti watakaokwenda kujenga hoja bungeni.
Mwalim amelsema, endapo atapata ridhaa ya kuongoza nchi, atahakikisha Bunge linakuwa na wabunge wenye uwezo wa kufanya utafiti ili kujenga hoja zenye tija kwa Taifa.
“Kama mbunge atakuwa na msaidizi mwenye uwezo mzuri wa kufanya utafiti, Bunge letu litakuwa la hoja, si la vihoja,” amesema.
Ameongeza kuwa wananchi wakichagua kwa mazoea, wataendelea kuongozwa kwa mazoea, hivyo aliwasisitiza wamchague mbunge anayefanya kazi, anayetoa hoja na kushika shilingi hadi hoja yake ipite.
Mwalim amewataka wakazi wa Urambo kutochagua kwa ushabiki bali kwa mabadiliko katika Uchaguzi Mkuu utakaofanyika Oktoba 29, mwaka huu.
Amesema kiwango cha umaskini na tatizo la ajira mkoani Tabora kinaongezeka, lakini wananchi bado wanaendelea kuikumbatia CCM licha ya kukosa maendeleo.
“Tangu dunia imeumbwa, Urambo ipo chini ya CCM, haijabadilika zaidi ya mikopo ya kausha damu. Badilikeni! Umaskini unakithiri, maisha ni magumu, halafu mnaichekea CCM — ikataeni,” amesema.
Mwalim amehoji mchango wa Urambo katika maendeleo, akisema:
“Mzee Samweli Sitta aliongoza Bunge vizuri na alijenga Bunge jipya, je, Urambo imefanyiwa nini?”
Amesema hana tatizo na Mama Magreth Sitta, lakini kama amechoka kisiasa ni heri atangaze kustaafu, kwani amekuwa madarakani kwa muda mrefu.
Amehitimisha kwa kuwataka wananchi wa Urambo kutofanya kosa katika uchaguzi huu, ili kupata majibu sahihi kuhusu dhahabu ya tumbaku na kuinua uchumi wa eneo hilo.

