Yasisitiza Walimu Kuwa Kioo Cha Jamii Kushiriki Katika Maamuzi Ya Maendeleo Ya Taifa
Na Lucy Ngowi
DAR ES SALAAM: CHAMA cha Walimu Tanzania (CWT) kimetoa wito kwa walimu na watanzania kwa ujumla kujitokeza kwa wingi kushiriki katika uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba 29, 2025, kikisisitiza umuhimu wa kutimiza haki ya kikatiba ya kuchagua viongozi bora watakaolinda maslahi ya wananchi.
Rais wa CWT Suleiman Ikomba ameeleza hayo alipozungumza na walimu.
Ikomba amesema ni wajibu wa walimu, kama kioo cha jamii, kuongoza kwa mfano kwa kuwahamasisha watanzania wote kushiriki kikamilifu katika uchaguzi huo muhimu.

“Ni lazima tuonyeshe mfano kwa jamii. Walimu ni kioo cha jamii, hivyo tunapaswa kuwahamasisha wananchi kutimiza haki yao ya msingi ya kupiga kura ili kuchagua viongozi watakaotuweka kwenye njia sahihi ya maendeleo,” amesema.
Ameongeza kuwa katika kipindi cha miaka mitano ijayo, CWT inalenga kuwa chombo kinacholeta matumaini mapya kwa walimu na kusaidia kuimarisha heshima ya taaluma ya ualimu nchini.
“Tunahitaji viongozi watakaoweka mbele maslahi ya walimu na kuifanya CWT kuwa chachu ya maendeleo kwa serikali na jamii. Serikali na jamii itaona CWT kama mshirika muhimu katika kuleta maendeleo ya nchi yetu,” amesema.
Chama hicho kimerejea dhamira yake ya kushirikiana na serikali na wadau wote wa maendeleo kuhakikisha walimu wanaendelea kuwa nguvu ya mabadiliko chanya katika jamii.

