Na Mwandishi Wetu, Kibaha
PWANI: CHAMA cha Wafanyakazi wa Serikali na Afya Tanzania (TUGHE) kimewataka wafanyakazi kote nchini kushiriki kikamilifu katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, mwaka huu 2025 kwa kuchagua viongozi watakaolinda na kusimamia maslahi yao.
Katibu Mkuu wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania (TUCTA), ambaye pia ni Katibu Mkuu wa TUGHE, Hery Mkunda ametoa rai hiyo katika kikao kazi cha wenyeviti na makatibu wa matawi ya TUGHE mkoa wa Dar es Salaam.

Mkunda amesema kushiriki uchaguzi ni wajibu wa kikatiba unaopaswa kutumika kwa busara.
“Siku ya uchaguzi tujitokeze kwa wingi, kwa sababu ni haki yetu ya kikatiba. Tuchague viongozi wanaojali maslahi ya wafanyakazi,” amesema.

Pia ameishukuru Serikali kwa hatua mbalimbali za kuboresha maslahi ya watumishi, ikiwemo kurejesha upandishwaji wa vyeo, kuongeza kima cha chini cha mshahara, na kuongeza siku za likizo kwa wazazi wanaojifungua watoto njiti.
Mkunda pia amewakumbusha viongozi wa matawi kufuata matakwa ya katiba ya chama kwa kufanya vikao vya tawi kama inavyotakiwa, akisema baadhi ya matawi yamekuwa hayatekelezi wajibu huo na hivyo kuwanyima wanachama fursa ya kushiriki maamuzi.

Awali, Mwenyekiti wa TUGHE mkoa wa Dar es Salaam, Brendan Maro, amemshukuru Mkunda kwa kufungua kikao kazi hicho, ambacho kinalenga kubadilishana uzoefu na kuimarisha uongozi wa chama katika maeneo ya kazi.




