Na Mwandishi Wetu
DODOMA: MKURUGENZI Mkuu wa Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA), Dkt. Erasmus. Kipesha amesema, mamlaka hiyo imefanikiwa kutekeleza miradi 3,768 yenye thamani ya Sh. Bilioni 49.5 katika kipindi cha mika minne ya serikali ya awamu ya sita.
Dkt. Kipesha amesema hay oleo Februari 2025 alipozungumza na Vyombo vya Habari kuelezea mafanikio na mipango yaTEA katika kipindi cha miaka minne ya Serikali ya Awamu ya Sita.
Amesema katika kipindi hicho, mamlaka hiyo imefadhili ujenzi wa vyumba vya madarasa, matundu ya vyoo, miundombinu kwa wanafunzi wenye mahitaji maalum, nyumba za walimu, mabweni, maabara za sayansi, na majengo ya utawala.
Pia amesema katika mwaka wa fedha 2024/2025, mamlaka hiyo kupitia Mfuko wa Elimu wa Taifa inaousimamia, imepanga kutekeleza miradi 113 yenye thamani ya Sh. Bilioni 11.3, ambayo itanufaisha wanafunzi 29,482.
Kwa maelezo yake, Miradi itakayofadhiliwa katika mwaka wa fedha 2024/2025 inajumuisha: ujenzi wa vyumba vya madarasa 45, ukarabati wa vyumba vya madarasa 11, ujenzi wa matundu ya vyoo 336, ujenzi wa nyumba za walimu 12, ujenzi wa mabweni nane na ununuzi wa vifaa vya TEHAMA kwa ajili ya shule tisa.
Vile vile amesema kiasi cha Sh. Bilioni tatu kitatumika kuimarisha miundombinu ya utoaji wa mafunzo ya amali, ikiwa ni sehemu ya kuwezesha utekelezaji wa mtaala mpya wa elimu nchini.
Akizungumzia michango kutoka kwa wadau, amesema Mamlaka imepokea michango yenye thamani ya Sh. Bilioni 4.11 katika kipindi cha miaka minne, kuanzia mwaka 2021/2022 hadi 2024/2025, pamoja na vifaa vyenye thamani ya Shilingi milioni 269.3.