Na Lucy Ngowi
MBEYA: JESHI la Zimamoto na Uokoaji mkoa wa Mbeya limetumia fursa ya maadhimisho ya Wiki ya Vijana Kitaifa yanayoendelea mkoani humo kutoa elimu ya kinga na tahadhari dhidi ya majanga ya moto kwa wananchi.
Akizungumza katika maonyesho hayo, Ofisa Habari Msaidizi wa Jeshi hilo, Sajenti Ester Kinyaga, amesema mikusanyiko mikubwa ya watu kwenye maeneo ya maonyesho ni fursa muhimu kwa Jeshi hilo kuelimisha jamii juu ya namna ya kujikinga na majanga ya moto na namna ya kutoa taarifa pindi ajali inapotokea.

“Tumekuja na vifaa mbalimbali tunavyotumia katika shughuli za uokoaji ili wananchi watakapofika kwenye banda letu wapate kujua kazi zetu kwa vitendo, pamoja na matumizi ya vifaa hivyo,” amesema.
Ametoa wito kwa wananchi kutembelea banda hilo ili kujifunza masuala muhimu kama ishara za moto, njia za kujikinga, na jinsi ya kutoa taarifa za dharura kwa kupiga namba 114, ambayo ni maalum kwa Jeshi la Zimamoto.
Akitaja baadhi ya visababishi vya majanga ya moto, amesema ni pamoja na uzembe wa kibinadamu na kutoa mfano, kwamba mtu anaacha pasi ya umeme ikiwa imeunganishwa baada ya umeme kukatika hivyo moto huweza kuzuka umeme unaporudi.

Pia hujuma inayosababishwa na mtu kumchomea mwenzake nyumba, gari au mali nyingine kwa makusudi kutokana na chuki au uhasama.
Amesisitiza kuwa elimu ya kinga dhidi ya majanga ya moto ni muhimu kwa kila mwananchi ili kuepusha hasara, majeraha au vifo vinavyoweza kuepukika.