Na Lucy Ngowi
DAR ES SALAAM: KATIBU Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu ( Sera, Bunge na Uratibu), Dkt. Jim Yonazi amekabidhi boti ya doria ya kukabiliana na vitendo vya kiuhalifu katika bahari na maziwa makuu nchini, kwa Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC),
Akikabidhi boti hiyo Dkt.Yonazi amesema doria hizo ni mwendelezo wa juhudi za serikali za kukabiliana na vitendo vya kiuhalifu ikiwemo uvuvi haramu na uhamiaji haramu.
Vitendo vingine vya kiuhalifu ni usafirishaji wa dawa za kulevya, biashara za magendo na utoroshwaji wa nyara za serikali.
“Hivyo ni matumaini yangu kuwa boti hii itatimiza lengo hilo na kuimarisha juhudiza serikali za kukabiliana na vitendo vya kihalifu katika eneo letu la bahari,” amesema.
Pia amesema serikali ina imani kubwa na uwezo wa TASAC katika usimamizi, uendeshaji na utunzaji wa boti hii. Hiyo ndiyo sababu iliyofanya boti hii kukabidhiwa kwa shirika hili.
“Ni imani yetu kuwa mtaitunza vizuri boti hii ikiwa ni pamoja na kuifanyia matengenezo kinga kwa wakati na hivyo kuwaongezea ufanisi katika kazi zenu za kila siku hususan katika ukaguzi kwa meli zinazoingia kwenye maji yetu ya ndani,” amesema.

Naye Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Uchukuzi Ludovick Nduhiye ameagiza TASAC, kuhakikisha boti hiyo inasimamiwa na wataalam wenye weledi, taaluma na uzoefu.
Pia ameagiza TASAC kuhakikisha boti inapata matengenezo ya kinga kwa kuzingatia ratiba itakayopangwa.
Vile vile kuhakikisha boti inakuwa na teknolojia ya kisasa na vitendea kazi vitakavyowezesha watumiaji kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi.
Awali Mkurugenzi Mkuu wa TASAC, Mohamed Salum amesema upatikanaji wa boti hiyo umefanyika katika wakati muafaka kwani utachagiza shughuli nyingi muhimu za utekelezaji wa vipaumbele vya Mradi wa Kukabiliana na Vitendo vya Kihalifu Bahari na Maziwa Makuu.
“Boti hii itasaidia utekelezaji wa majukumu ya TASAC iliyokasimiwa kisheria, hususan jukumu la usimamizi wa usalama, ulinzi na utunzaji mazingira dhidi ya uchafuzi utokanao na shughuli za meli.
“Boti tunayokabidhiwa leo itasaidia utekelezaji wa jukumu hili,”amesema.