Na Mwandishi Wetu
KATIBU Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mary Maganga ameuagiza Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF) kuhakikisha inazingatia ubora wa huduma inazotoa kwa wananchi ili kuendana na ithibati ya utoaji wa huduma kwa viwango vya kimataifa iliyoupata.
Maganga ameyasema hayo jijini Dar es Salaam wakati wa hafla ya WCF kukabidhiwa Cheti cha Ithibati ya utoaji wa huduma bora kwa viwango vya kimataifa.
Maganga amesema maboresho yanayofanywa na mfuko huo yanapaswa kuzingatia mahitaji na matarajio ya wateja wake ili kuhakikisha wafanyakazi wanapatiwa haki yao ya fidia stahiki pale wanapopatwa na madhila yatokanayo na kazi zao.
Amesema hayo wakati akikabidhi cheti hicho kwa Mkurugenzi Mkuu wa WCF, Dkt. John Mduma.

“Kitu cha msingi ni kuhakikisha mnaendelea kuboresha mifumo ya utoaji wa huduma zenu. Nasisitiza mtumie ithibati hii mliyoipata kurahisisha taratibu za kuwasajili waajiri ili ikiwezekana waweze kujisajili wenyewe kwa hiari badala ya kulazimishwa kufanya hivyo kwa mujibu wa sheria,,” amesema.
Katibu Mkuu huyo ameongeza kuwa jitihada za kutoa elimu kwa wadau wake pamoja na kutumia matokeo ya tafiti mbalimbali ili kuhakikisha huduma zake zinakidhi mahitaji ya wateja ni muhimu kuzingatiwa.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa WCF, Dkt. Mduma amesema kuwa mafanikio waliyoyapata yamechangiwa kwa kiasi kikubwa na uwekezaji mkubwa wanaofanya katika matumizi ya mifumo ya Tehama.
Ametoa rai kwa wadau wa Mfuko huo kutumia huduma za mtandao katika kupata huduma mbalimbali zitolewazo na WCF.
“Tumewekeza katika matumizi ya Tehama, ambapo kwa sasa takribani asilimia 90 ya huduma za Mfuko zinapatikana kwa njia ya mtandao ikiwemo usajili, kutoa taarifa ya madhila kutokana na kazi na kurekebisha taarifa za wafanyakazi.
“Kwa kufanya hivyo tutakuwa tunaoishi maono ya Rais Samia Suluhu Hassan, aliyeelekeza kwamba mifumo ya taasisi zote ni vyema isomane ili kuleta ufanisi katika utoaji wa huduma kwa wananchi,” amesema.
Naye Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Viwango Tanzania (TBS) Viola Masako ameipongeza WCF kwa juhudi kubwa za utendaji hadi kufikia mafanikio hayo yanayoonesha nia thabiti ya Mfuko kuwajibika katika utoaji wa huduma kwa wateja wake kwa viwango vya kimataifa.
“TBS tunaipongeza WCF na tumeshukuru kwa jambo hili kwa sababu linatuongezea wigo wa kuisaidia Serikali yetu kutekeleza majukumu yake kwa wakati na pia kujipima namna ya kuboresha zaidi utoaji wa huduma zake kwa wananchi,” amesema.

WCF ni Taasisi ya Hifadhi ya Jamii iliyochini ya Ofisi ya Waziri Mkuu yenye jukumu la kutoa fidia kwa wafanyakazi wanapoumia, kuugua kutokana na kazi wanazozifanya kwa mujibu wa mikataba ya ajira zao na pale mfanyakazi anapofariki kutokana na kazi wategemezi wa familia yake hulipwa fidia na WCF.