Na Lucy Ngowi
GEITA: BENKI Kuu ya Tanzania (BoT) imetunukiwa tuzo ya kutambua mchango wake katika kudhamini Maonesho ya Nane ya Teknolojia ya Madini yanayoendelea mkoani Geita.
Tuzo hiyo imetolewa na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa na kupokelewa na Meneja wa Idara ya Mawasiliano wa BoT, Victoria Msina, leo Septemba 22, 2025, katika Viwanja vya Dkt. Samia Suluhu Hassan vilivyoko Bombambili, Geita, ambapo Waziri Mkuu alifungua rasmi maonesho hayo.

BoT inashiriki katika maonesho hayo kwa lengo la kutoa elimu ya kifedha kwa wananchi pamoja na kusaidia kutatua changamoto mbalimbali zinazowakabili.
Maonesho hayo, yaliyoanza Septemba 18, 2025, yamekusanya washiriki zaidi ya 600 kutoka ndani na nje ya nchi, wakiwemo wafanyabiashara, wananchi na wadau wa sekta ya madini, wakionesha teknolojia mbalimbali zinazotumika katika sekta hiyo.
Haya yamekuwa jukwaa muhimu kwa Serikali, sekta binafsi, wachimbaji wa madini wa viwango vyote, taasisi za kifedha, wajasiriamali na wadau wengine kujadiliana, kubadilishana uzoefu na kujifunza kutoka kwa wenzao.
Kaulimbiu ya maonesho kwa mwaka huu ni: “Ukuaji wa Sekta ya Madini ni Matokeo ya Matumizi ya Teknolojia Sahihi na Uongozi Bora. Shiriki Uchaguzi Mkuu Oktoba, 2025.”