Na Danson Kaijage
DODOMA: WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa amewataka watanzania kujenga utamaduni wa kufanya mazoezi kama sehemu ya kuhimarisha afya zao pamoja na kuchangia mambo ya kimaeendeleo.
Majaliwa ameeleza hayo wakati akizungumza na wabunge, wadau wa Maendeleo na watanzania wa rika mbalimbali kwenye hitimisho la Bunge Marathon lililokuwa likilenga kuchangisha zaidi ya Sh. Bilioni tatu kwa ajili ya kujenga shule ya wavulana ya bweni ya Kidato cha tano na sita katika Kata ya Kikombo Jijini Dodoma.
Amesema Bunge kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wa maendeleo pamoja na wananchi, wamefanya jambo hilo kuhamasisha watanzania kujenga shule ya mfano ya bweni ya wavulana ambayo itakuwa na huduma muhimu za kitaaluma na kuwafanya wanafunzi watakaojiunga na shule hiyo kufurahia masomo watakayo patiwa shuleni hapo.

“Shule itakuwa na maabara nne za kisasa, itakuwa na mabweni ya uwezo wa kulaza wanafunzi 300, maktaba kubwa na ya kisasa,nyumba za walimu pamoja na viwanja vya michezo.
“Shule hii inajengwa baada ya Bunge kujenga shule ya kisasa ya mfano ya wasichana ambayo kwa sasa matokeo yake yanaonekana na hii ni kuonesha kuwa serikali inawajali watoto wa kike na kiume,” amesema.
Amesema ujenzi wa Shule hiyo ni mwendelezo wa ujenzi wa shule za kike za watoto wenye mahitaji maalumu pamoja na uboreshaji na uandaaji wa mfumo wa TEHAMA na kuzifanya kutoa masomo ya Amali.

Naye Spika wa Bunge Tullia Akson amesema Bunge linaendesha michango kwa ajili ya kuwekeza katika elimu kama sehemu ya alama ya Bunge.
“Sisi wabunge tunatambua umuhimu wa watoto wa kike na kiume hivyo sasa tunahitaji kujenga shule ya kisasa ya wavulana ambayo itakuwa na ubora unaokubalika kitaaluma,”amesema .