Na Mwandishi Wetu
NAIBU Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe.Dkt. Doto Biteko amezitaka taasisi za ufutiliaji na tathmini kufanya kazi kwa weledi na kuimarisha eneo hilo ili kuendana na mahitaji yanayolenga kuleta tija katika utoaji wa huduma kwa wananchi.
Hayo yameelezwa leo Septemba 20, 2024 Zanzibar na Dkt. Biteko wakati akimwakilisha Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa katika Kongamano la Tatu la Ufuatiliaji, Tathmini na Kujifunza.
Amesema wataalam wa ufuatiliaji na tathmini wanawajibika kuilinda taaluma hiyo na kuwashawishi kwa hoja wakuu wa taasisi husika kupenda kazi zinazotokana na taaluma hiyo badala ya kujisikia wanyonge kitaaluma.
Aidha, Dkt. Biteko amewataka washiriki muda wote kusisitiza misingi ya taaluma hiyo na baadaye kuleta matokeo chanya kwa maendeleo ya Taifa na watu wake.
“Inawezekana katika maeneo yenu ya kazi wakawepo wakuu wa taasisi au viongozi wa serikali ambao hawapendi mfanye kazi yenu vizuri, kukubaliana na hilo ni kujiua wenyewe. Mnapotoka hapa mkafanye mkuu wa taasisi au kiongozi aone umuhimu wenu katika shirika.” Amesema Dkt. Biteko.
Aidha, amewataka wataalamu hao kusema ukweli na kusimamia taaluma yao.
“ Nataka niwaombe mkajiamini Rais Samia ameahiza na kuelekeza uwepo wa vitengo mbalimbali
mfuatilie fedha zinazopelekwa kwenye miradi na matokeo yake kwenye kubadilisha hali za maisha ya watu.” Amesisitiza Dkt. Biteko.
Kupitia kikao hicho, ametoa maagizo matano yakilenga kuboresha ufuatiliaji, tathmini na kujifunza.
Aidha ameielekeza Ofisi hiyo kukamilisha Sera ya Kitaifa ya Ufuatiliaji na Tathmini ili iwezeshe utekelezaji sahihi wa eneo la ufuatiliaji na tathmini nchini.
Kwa upande wake, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge na Uratibu, William Lukuvi amesema Kongamano hilo la tatu la Ufuatiliaji, Tathmini na Kujifunza.
Amesema kauli mbiu ya kongamano ni ‘Kuimarisha utoaji wa huduma kwa wananchi kwa kutumia teknolojia katika ufuatiliaji na tathmini na matumizi ya matokeo ya tathmini katika kufanya maamuzi’ limepata mwitikio mkubwa kutoka kwa wadau na washiriki.
Ametaja lengo la Kongamano hilo kuwa ni kuweka msisitizo kwenye lengo kuu la Serikali la kutoa huduma bora na kwa wakati kwa wananchi .
Naye, Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge na Uratibu, Dkt. Jim Yonazi amesema kupitia Kongamano hilo wamepata fursa mbalimbali ikiwemo kuwa na mchango mkubwa katika kuongeza uwezo wa wataalamu.
“ Kongamano hili limesisitiza umuhimu wa wananchi kushiriki katika mchakato mzima wa Ufuatiliaji na Tathmini ili kuimarisha uwazi, uwajibikaji na kuhakikisha Serikali na wahisani wanatoa huduma zenye tija. .” Amesema Dkt. Yonazi.
.