Na Lucy Lyatuu
JESHI la Polisi kwa kushirikiana na mamlaka nyingine za kisheria ikiwemo Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) wamewakamata watuhumiwa 25 wanaojihulisha na makosa ya kimtandao katika maeneo mbalimbali ya Dar es Salaam na mikoa mingine.
Kamanda wa Polisi, Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Jumanne Muliro amesema hayo Dares Salaam na kuongeza kuwa watuhumiwa hao ni pamoja na Kelvin Sauro mkazi wa Ifakara na wenzake 14.
Amesema wanatuhumiwa kuongoza kikundi cha kihalifu mtandaoni, kutumia laini za simu zisizo na usajili wao, kuingilia na kubadili namba za utambuzi halisi wa simu, (IMEI) kujipatia pesa kwa njia ya udanganyifu na kujifanya maofisa wa mfuko wa pensheni na kuwaibia wastaafu.
Kamanda Muliro amesema pia wanatenda makosa ya utakatishaji wa fedha.
Amesema watuhumiwa wamekuwa wakituma jumbe kama “tuma ile hela kwa namba hii’’ ‘’tuma kwenye namba hii ile pesa ya kodi’’. ‘Leta no za NIDA, Vitambulisho tukushughulikie mapunjo yako ya kustaafu’
Aidha amesema Jeshi hilo limemshikilia pia Enrique Adolph Ngagani na wenzake wanne wa Sinza Kinondoni Dar es Salaam kwa tuhuma za kumiliki akaunti za mtandao wa Tiktok zinazotumika kusambaza taarifa zenye maudhui ya udhalilishaji wa watu mbalimbali kupitia Program za akili Unde (Artificial Intelligence – AI).
Amesema akametwa na kushikiliwa pia Baruani Hamisi Kateme maarufu kama Majani mkazi wa Kahororo Mkoa wa Kagera na wenzake wanne kwa tuhuma za udanganyifu na utapeli kwa wastaafu na kuwaibia fedha kwa kujifanya kuwa ni wafanyakazi wa Mifuko ya pensheni na kuwa anashughulika na mapunjo ya wastaafu.
Amesema baadhi ya watuhumiwa wamekamatwa wakiwa na vifaa vya elekroniki kuhusiana na makosa yao kama simu janja 10, simu za kawaida 26,laini za simu 84 za kampuni mbalimbali, Memory cardy mbili, kompyuta mpakato moja, mashine ya kusajili laini mbili,gari na funguo moja.
Amesema baadhi ya watuhumiwa tayari wamefikishwa mahakamani Kisutu na wengine taratibu za kisheria zinakamilishwa ili wafikishwe mahakamani.
Kamanda Muliro amesema Jeshi hilo linatoa wito kwa wananchi kufuata sheria na kanuni za matumizi ya mitandao pia kuwatahadharisha wananchi kutokutoa vitambulisho vyao kama vya NIDA na vingine kwa watu wasiowajua.
Aidha amesema Polisi inatoa onyo kali dhidi ya wote wanaojihusisha na makosa ya kimtandao na mengine kwani watu hao watashughulikiwa vikali lakini kwa mujibu wa sheria.