Na Lucy Lyatuu
WATANZANIA wametakiwa kulinda viwanda vya ndani ya nchi pamoja na kutumia bidhaa zinazotengenezwa humo ili kuviwezesha kuendelea na uzalishaji, kuongeza ajira, na kukuza uchumi kwa ujumla.
Waziri wa. Viwanda na Biashara, Dk Selemani Jafo amesema hayo akiwa ziarani mkoa wa Kilimanjaro na kuwataka Watanzania kulinda viwanda vya Serikalli kwa kufanya kazi kwa uadilifu, weledi, uzalendo na hofu ya Mungu ili kiepuka kusababisha uharibifu unaoweza kutokea.
Amesema Serikali imewekeza fedha nyingi kuvifufua viwanda hivyo na kuviendesha .
Akiwa katika ziara hiyo ametembelea viwanda, kuongea na Wafanyabiara pamoja na Maofisa Biashara wa Mkoa huo kwa lengo la kujionea shughjuli za uzalishaji, kusikiliza changamoto na kuona njia bora ya kuzitatua kwa kushirikiana na taasisi nyingine .
Aidha, Waziri Jafo akiwa mkoani humo ametembelea Kiwanda cha Kutengeneza Vinywaji baridi cha Kiwanda cha A One product and Bottles Ltd, Kiwanda cha Bonite Bottlers Ltd, Kiwanda cha kutengeneza bidhaa za ngozi cha Kilimanjaro, Kiwanda cha kutengeneza vipuri na mitambo mbalimbali cha KMTC, Eneo la uwekezaji la bustani ya wanyamapori ya Serval (Serval Wildlife) pamoja na Kiwanda cha Sukari Moshi (TPC).
Akiwa katika Eneo la uwekezaji la bustani ya wanyamapori ya Serval (Serval Wildlife) Dkt. Jafo amewahimiza Watanzania kutumia muda wao wa mapumziko kufanya utalii wa ndani ili kukuza biashara ya utalii na kuvutia wafanyabiashara katika sekta hiyo.
Katika hatua nyingine akiongea na Wafanyabiashara na Wamiliki wa Viwanda wa Mkoa wa Kilimanjaro, Waziri Jafo amewataka Watumishi wa Umma Mkoani humo kiwasaidia wafanyabiashara na amewaahidi kuwa atashirikiana na Taasisi nyingine za kisekta kutatua changamoto zilizopo kwa lengo la kuendelea kuweka mazingira bora ya biashara.
Vilevile Dkt Jafo amehamasisha utekelezaji wa Mpango wa Viwanda Tqnzania unaoelekeza kuwa kila Mkoa unapaswa kuanzisha Viwanda vikubwa vitatu, Viwanda vya kati vitano , Viwanda vidogo 20 na Viwanda vidogo sana 30 ili kukukuza sekta ya viwanda kuongeza ajira na pato la Taifa
Naye Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro na Mkuu wa Wilaya ya Rombo Raymod Mwangala ameahidi kwa Mkoa wa Kilimanjaro utaendelea kufufua viwanda vya zamani visivyofanya kazi na kuanzisha vipya ili kiongeza ajira na pato la taifa mkoani humo.