WATAFITI wa mradi wa Mbinu Shirikishi za Wanafunzi na Wakulima katika Uvumbuzi na Uhaulishaji wa Maarifa na Teknolojia za Kilimo (AGRISPAK) kutoka Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) wameanza utekelezaji wa mpango wa uandaaji wa vitabu vidogo.
Vitabu hivyo vina lengo la kutoa majibu ya changamoto mbalimbali za wakulima nchini kwa kuwapatia mafunzo wanafunzi watafiti watakaoshiriki kwenye kuandaa vitabu hivyo.
Akifungua mafunzo hayo Mkuu wa Mradi wa AGRISPARK, Dkt. Philbert Nyinondi amewataka wataalamu kuzingatia mafunzo hayo ya awali ambayo yana lengo la kuwajengea msingi wa kazi ambayo wanatarajia kuanza kuifanya.
“Kwanza niwapongeze kwa kupata nafasi ya kushiriki kwenye kufanya kazi hii muhimu kati ya wanafunzi wengi wa Chuo chetu,
“Mtambue kuwa kazi hii mnayoifanya ni kwa maslahi ya wakulima na wafugaji wetu maana vitabu mtakavyoandaa tunatarajia vitasaidia kujibu changamoto mbalimbali wanazokabiliana nazo wakulima na wafugaji na vitasambazwa kwa njia mbalimbali kuwafikia ikiwemo kupitia mfumo wa MKULIMA LIBRARY uliopo kwenye Maktaba ya Taifa ya Kilimo,” amesema.
Mkuu huyo wa mradi wa AGRISPARK amesema baada ya mafunzo hayo watapata nafasi ya kwenda kwenye maeneo mbalimbali ya mradi ikiwemo Wilaya ya Mvomero, Manispaa ya Morogoro na Halmashauri ya Wilaya ya Morogoro Vijijini kwa ajili ya kukutana na wakulima,
Pia kuzungumza nao katika mazingira halisi ili kupata taarifa mbalimbali kuhusu mada za vitabu wanavyoviandaa.
Pia Dkt. Nyinondi amewataka kuzingatia mambo mbalimbali wakutanapo na wakulima vijijini ikiwemo suala la matumizi sahihi ya lugha ya Kiswahili kwa kutochanganya na lugha ya kiingereza kwenye mazungumzo yao.
Vile vile kwenye mavazi, maadili ya jamii husika pamoja na kutowaona wakulima kama hawajui bali watambue kuwa wana uzoefu wa miaka mingi na wanajua vitu vingi ambavyo wao hawajui.
Kwa upande wake Mtafiti Mkuu Mwenza wa Mradi huo wa AGRISPARK Dkt. Nicholaus Mwalukasa amesema wakati wa mafunzo hayo watapitishwa kwenye mada mbalimbali ili kuwajengea uwezo katika kutekeleza kwa ufanisi zoezi hilo.
Ikiwemo mnyororo wa thamani wa mazao mbalimbali, kilimo bora cha mazao, masuala ya masoko, Mbegu bora za kilimo pamoja na namna ya kuandaa vitabu hvyo.
“Mafunzo haya tumeona ni muhimu sana kwenu kufanyika kabla ya kuanza kazi kubwa iliyo mbele yenu, na tunaamini baada ya mafunzo haya na kuelewa upana wa kazi hii na matarajio ya mradi mtaweza kufanya kazi nzuri ambayo itakuwa na mchango mkubwa kwa wakulima wetu na taifa kwa ujumla wake,” amesema.
Dkt. Mwalukasa amesema kazi inayofanyika ni sehemu ya utekelezaji wa malengo ya mradi huu ya kutumia mbinu Shirikishi za wanafunzi na wakulima katika Uvumbuzi na Uhaulishaji wa Maarifa na Teknolojia za Kilimo kwa kutengeneza vijitabu vizuri ambavyo vitasaidia kufikia lengo hilo.
Akizungumza kwa niaba ya washiriki wenzake Hawa Twaibu amewahakikishia viongozi wa mradi huo na SUA kuwa watafanya kazi kwa bidii katika kuhakikisha wanatimiza malengo ya mradi kwa wakati na kwa ufanisi mkubwa katika kipindi chote watakachukuwa kwenye zoezi hilo.
“Tunashukuru Mradi wa AGRISPARK na Chuo kwa kutupa nafasi ya kufanya kazi hii muhimu kwa wakulima wa Tanzania,
‘Na tunaamini kupitia kazi hii itatupatia uzoefu mkubwa kwenye kuteleza mazoezi ya aina hii siku zijazo na kutusaidia kuweza kujua namna ya kufungasha elimu na kuifikisha kwa wakulima na wahitaji wengine,” amesema.
Mradi wa AGRISPARK Ulizinduliwa mwishoni mwa mwaka jana 2024 na Rasi wa Ndaki ya Sayansi Asilia na Tumizi (CoNAs) Dkt. Geofrey Karugila kwa niaba ya Makamu Mkuu wa Chuo hicho Profesa Raphael Chibunda.
Unafadhiliwa na Serikali kupitia SUA kama maono makubwa ya Chuo katika kuinua watafiti wake hasa wachanga kwa kutenga fedha za ndani ili wafanye tafiti za kusaidia kutatua changamoto za jamii na taifa.