Na Lucy Lyatuu
WASTAAFU Wa Jeshi La Polisi nchini wameshauriwa kutumia vyema mafao wanayopata na kuwaona watalaam watakaowangoza kwenye kazi wanazoweza kuzifanya.
Mkuu wa Taasisi Ya Uhasibu Tanzania( TIA) Profesa William Pallangyo amesema hayo katika sherehe za kuwaaga Wastaafu nane wa Chuo Cha Taaluma Ya Polisi Dar es Salaam Chuo hicho na kuwaambia kuwa kustaafu sio mwisho Wa Maisha Bali ni wakati wa kushiriki shughuli za kujenga Taifa.
Amewataka kutumia busara katika kupanga maisha na matumizi ya mafao, huku wakilinda afya na kushirikiana kwa karibu na familia zao.

“Zaidi ya hayo, endeleeni kuwa kiunganishi bora kati ya Jeshi la Polisi, Serikali na wananchi,”amesema na kuongeza kuwa kwa wale waliopata mikataba ya kuendelea na utumishi, wafanye kazi kwa bidii wakithibitisha kwamba bado taifa linahitaji maarifa na hekima yao.
Amesema wastaafu wana tabia ya kukata tamaa,na kuwataka kuwa isiwe hivyo.
Aidha amesema TIA Ina mpango Wa kuanzia Kutoa shahada ya Polisi sayansi ambapo watawashirikisha Wastaafu katika kufanikisha suala hilo.

Amesema kwa upande wa wapiganaji ambao bado wapo kazini, kitendo cha kuwaaga wengine kiwe darasa na kioo cha kujiangalia huku wakijiandaa mapema kwa maisha ya kustaafu.
“Kila mmoja akumbuke kwamba wakati wake nao unakuja, hivyo ni vyema kujiandaa kwa nidhamu, weledi na mipango ya busara,” amesema.
Wakati huo huo alimpongeza Mkuu wa Jeshi la Polisi Tanzania, (IGP) Camillius Wambura, ambaye alihakikisha Wastaafu hao wanapata mafunzo ya msingi, malezi ya taaluma ya kazi na dira ya utumishi yenye uadilifu na weledi wa kipolisi.
Kwa upande wake Mkuu wa Chuo hicho Dkt. Lazaro Mambosasa Naibu Kamishna wa Jeshi la Polisi, amesema anatambua mchango wa Wastaafu hao na kusisitiza kuwa kustaafu sio mwisho bali ni wakati wanaohitaji kuwa na matumizi mazuri ya muda,kutulia na wenzi wao kwa malezi bora na uongozi makini .

Amesema fedha ya kustaafu sio madini hivyo watulie na familia zao wakikumbushana walivyokutana Kwa Mara ya kwanza huku wakiweka Mipango ya pamoja ya usimamizi Wa miradi itakayofanyika.