Na Lucy Ngowi
DAR ES SALAAM: NAIBU Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji Stanslaus Nyongo amesema suala la ulipaji kwa kutumia fedha taslimu ni tatizo hivyo ameshauri ulipaji kodi ufanyike kwa njia ya mtandao.
Nyongo amesema hayo wakati akifungua Kongamano la Kwanza la Kodi katika Hoteli ya Rotana Dar es Salaam.

Amesema endapo itahimizwa na wananchi wakatumia teknolojia ya ulipaji kodi kimtandao itakuwa nzuri.
“Tukisema petrol station zote zilipe kimtandao sio cash ( taslimu), nini kitashindikana? Shida ipo wapi? Mtu mwenye boda, basi, Lori, anashindwa nini kulipa pesa kimtandao?
“Masuala ni kuamua tu, leo tujadili tushikamane kwa pamoja,” amesema.

Amewataka watunga sera, wafanya biashara, watafiti na wataalam wa kodi kwa ajili ya kujadili mikakati ya kupanua wigo wa kodi na kuimarisha ulipaji kodi kwa hiari ili kuongeza mapato ya serikali wakae na kufikiria na kuangalia wafanye nini.
Pia amesema urasimishaji biashara upo chini kwa kiwango kidogo, anayefanya biashara bila kulipa kodi anaonekana ananufaika zaidi.
“Ni vema watu wakaelimishwa na kuona kulipa kodi ni jambo la kifahari,” amesema na kuongeza kuwa kongamano hilo ni muhimu katika kuongeza uelewa katika masuala ya ukipaji kodi.
“Leo tutapata elimu ya kutambua namna gani tutaweza kufanya biashara. Leo tunaweza kutoka hapa na yale mambo yatakayo turahisishia kuweza kukusanya kodi,” amesema.
Ameongeza kuwa kwa kutumia fursa ya kongamano wataongeza uelewa bila kutumia nguvu nyingi.
Amesisitiza kuheshimiwa kwa michango ya wadau na kusema, ” Tumekuwa na tatizo kubwa kwani watu wamekuwa wanatoa michango yao lakini haichukuliwi wala kufanyiwa kazi,”.
Kwa upande wake Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania ( TRA), Yusuph Mwenda amekipongeza Chuo cha Kodi kwa kuandaa kongamano hilo ambalo litasaidia mamlaka hiyo kuendelea kupata mawazo ya kuboresha.
” Kongamano linaenda kuboresha jukumu la TRA kwa kushauri isimamizi wa kodi,” amesema
Amesema kongamano hilo ni fursa ya kupata mrejesho kwa kusikiliza wapi wanakosea, wapi wameboresha na kuangalia ni namna gani wataweza kuongeza wigo wa kodi huku biashara zikikua.
“Sekta isiyo rasmi ni kubwa sana natarajia tuzungumze tutaibadilishaje walipe kodi,” amesema.
Naye Mkuu wa Chuo cha Kodi ( ITA), Profesa Isaya Jairo amesema matarajio ya kongamano hilo kwa wadau ambao ni walipa kodi, wafanya biashara, wataalamu wa kodi wataweza kujadili na kutoa majawabu.
“Kwa majadiliano hayo wataweza kuongeza wigo sio mpana na watu hawalipi kodi na wengine hawalipi jlkodi stahiki.
“Tujadiliane na wadau tujue watawezaje kulipa kodi ya serikali,” amesema.