Na Lucy Ngowi
DAR ES SALAAM: WANANCHI wengi nchini wanakumbwa na changamoto ya kutokujua utaratibu sahihi wa kuwasilisha malalamiko yao dhidi ya ukiukwaji wa maadili unaofanywa na baadhi ya maofisa wa mahakama, jambo linalokwamisha upatikanaji wa haki kwa wakati.
Akizungumza jijini Dar es Salaam, Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini katika Tume ya Utumishi wa Mahakama, Lidya Churi amesema changamoto hiyo inatokana na uelewa mdogo miongoni mwa wananchi kuhusu majukumu ya Tume pamoja na kamati zake za maadili.
“Tume ya Utumishi wa Mahakama inatekeleza majukumu muhimu ya kusimamia maadili ya maofisa wa mahakama, lakini bado wananchi wengi hawajui ni wapi wanapaswa kuelekeza malalamiko yao. Hali hii inaweza kusababisha kuwepo kwa malalamiko ambayo hayawasilishwi,” amesema

Amesema pamoja na kuwepo kwa mifumo ya kushughulikia malalamiko, ukosefu wa uelewa kuhusu kazi na mamlaka ya tume umekuwa kikwazo kikubwa katika kuhakikisha uwajibikaji na utoaji wa huduma bora kwa wananchi kupitia vyombo vya utoaji haki.
Churi amesisitiza kuwa ili wananchi waweze kufaidika ipasavyo na huduma zitolewazo na mahakama, ni muhimu kwao kufahamu kazi zinazofanywa na Tume ya Utumishi wa Mahakama, pamoja na kamati zake, ikiwemo Kamati ya Maadili.
Ametoa wito kwa taasisi za habari na wadau wa sheria kushirikiana katika kutoa elimu kwa umma kuhusu utendaji wa Tume na namna ya kuwasilisha malalamiko ya ukiukwaji wa maadili kwa mujibu wa taratibu zilizowekwa kisheria.
“Wananchi wana haki ya kupata huduma ya haki kwa wakati, na hii inawezekana tu iwapo wataelewa mifumo ya uwajibikaji iliyo ndani ya mahakama zetu,” amesema.
Tume ya Utumishi wa Mahakama ni chombo huru kilichoanzishwa kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, chenye jukumu la kuhakikisha kuwa utumishi ndani ya mahakama unaendeshwa kwa weledi, uwazi na kwa kuzingatia maadili ya taaluma ya sheria.